
Dkt. Tulia Ackson
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
-------------
Aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Tulia Ackson, jana Novemba 7, 2025 alitangaza kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi hiyo.
Hata hivyo, Dkt. Tulia ambaye pia alikuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), hakuweka wazi sababu za kujiondoa kwake katika kinyang’anyiro hicho.
Dkt. Tulia alikuwa miongoni mwa majina yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma Novemba 5, 2025, baada ya kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.
Wengine walioteuliwa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ni Mussa Azzan Zungu na Stephen Julius Masele. Kwa upande wa nafasi ya Naibu Spika, walioteuliwa kuwania ni Najma Giga, Daniel Sillo na Timotheo Mzava.
Hivyo, baada ya Dkt. Tulia kujiondoa, wagombea waliobaki katika kinyang’anyiro hicho ni Mussa Zungu na Stephen Julius Masele, ambao sasa wanaendelea na hatua za ndani ya chama kuelekea kupigiwa kura.
Dkt. Tulia alichukua kijiti cha Uspika mwaka 2022 kutoka kwa Job Ndugai ambaye baadaye aliyeng’atuka kwenye nafasi hiyo.
Kabla ya hapo, alikuwa Dkt. Tulia alikuwa Naibu Spika kuanzia mwaka 2015, baada ya kuteuliwa na Rais wa wakati huo, Dkt. John Magufuli, kuwa mbunge kabla ya kugombea nafasi hiyo aliyodumu nayo hadi mwaka 2020, na kuendelea hadi alipoteuliwa kuwa Spika mwaka 2022.
Umaarufu wa Dkt. Tulia katika ulingo wa siasa ulianza mwaka 2014 baada ya kuteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Hata hivyo, jina la Dkt. Tulia lilivuma zaidi Oktoba 2015 alipoteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kabla ya kuingia rasmi katika siasa za uchaguzi.
No comments:
Post a Comment