NEWS

Saturday, 22 November 2025

FZS Tanzania yazindua Mfumo mpya wa Kupokea, Kutatua Malalamiko ya Wananchi kuhusu miradi yake




Na Mwandishi Wetu
Akiripoti kutoka
Serengeti
--------------

Novemba mwaka huu, Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) Tanzania lilizindua awamu ya pili ya Mfumo mpya wa Kupokea na Kushughulikia Malalamiko ya Jamii kuhusu shughuli za uhifadhi na ushirikiano katika wilaya ya Serengeti.

Uzinduzi huo ulifanyika kupitia warsha zilizohusisha vijiji vitano Bonchugu, Robanda, Bokore, Makundusi na Merenga, ambapo wawakilishi wa jamii kupitia wajumbe wa halmashauri ya vijiji walipata nafasi ya kujifunza na kueleza changamoto zao.

Septemba mwaka huu, katika awamu ya kwanza ya mchakato wa kuanzisha Mfumo wa Kupokea na Kushughulikia Malalamiko ya Jamii, FZS ilikutana na wadau wakuu wa uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) - Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mapori tengefu ya Ikorongo na Grumeti, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ikona.

Katika warsha hiyo, Shirika la FZS lilipokea ushauri wa kitaalamu, ambapo wadau hao waliweka msingi wa pamoja juu ya umuhimu wa mfumo rasmi, shirikishi na salama wa kupokea malalamiko, wakitumia mifano halisi ya kitaifa na changamoto zilizojitokeza kwenye miradi ya uhifadhi kama rejea muhimu ya kuweka tahadhari mapema.

Majadiliano yao yaliweka wazi kwamba jamii za Serengeti zinahitaji daraja la kudumu kati yao na taasisi za uhifadhi, na mfumo huo ndio njia ya kuhakikisha uwazi, ushirikishwaji na ufuatiliaji wa malalamiko kwa mujibu wa sheria na haki za binadamu.

Katika warsha hiyo ya mafunzo awamu ya pili, Afisa Ulinzi wa Jamii wa FZS Tanzania, Digna Irafay, alieleza kwamba mfumo huo mpya, umeundwa ili kuwa njia salama, ya uwazi na haki kwa wananchi kutoa malalamiko yao, kuuliza maswali na kushiriki katika ufuatiliaji wa masuala yanayogusa maisha yao na shughuli za miradi ya FZS.

Irafay alisisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha “wananchi wanapata haki yao ya kushirikishwa kwenye miradi inayohusi rasilimali muhimu kwa urahisi, usawa na kusikilizwa kupitia mchakato unaoheshimu haki za binadamu, na kwamba kila sauti ya mwananchi inasikilizwa.”

Kwa mujibu wa mfumo huo, Afisa Miradi ya Jamii na Uhifadhi, Nelson Olekwai (FZS) kutoka programu ya Sengereti, alieleza kuwa malalamiko hutokana na changamoto kama kukosekana njia rasmi ya kutoa taarifa, makundi maalum kuachwa nyuma, uvumi na taarifa zisizo rasmi, na kukosekana kwa mawasiliano kati ya jamii, vijiji, wilaya na wadau wengine.

Mfumo unaweka njia ya wazi kabisa kuhusu hatua za kijiji, mradi na Kamati ya Malalamiko katika kile kilichoelezwa kama “njia salama ya kutatua matatizo kabla hayajawa migogoro.”
Kwa upande wake, Afisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, John Lendoyan, aliwataka viongozi wa vijiji, hasa Bonchugu, ambacho ndicho kijiji cha kwanza kufikiwa, kuwa mabalozi wazuri wa mfumo huo na kutoa ushirikiano kwa FZS ili lengo la mfumo huo lifanikiwe.

Alieleza kwamba ili kupata haki, wadau wote wana jukumu la kuhakikisha kuwa mfumo huo unatumika kwa tija ya kuongeza ubora wa miradi ya uhifadhi kwa jamii.

Washiriki wa warsha kutoka vijiji vyote vitano walipongeza mfumo huo mpya, wakisema utaboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uhifadhi.

Nchagwa Marwa, mshiriki kutoka Bonchugu, alisema: “Ni mfumo mzuri. Utaboresha huduma hata kwa makundi maalum kama wanawake, vijana, watoto, wazee, yatima na watu wenye ulemavu. Nitapeleka elimu hii kwa kikundi changu cha COCOBA (Community Conservation Banks).”

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bonchugu, Simon Mahando, aliongeza kuwa mfumo huo utapunguza migogoro isiyo ya lazima na kueleza kuwa ni nafasi nzuri kwa jamii kutoa sauti zao moja kwa moja.

Mjumbe kutoka kijiji cha Makundusi alishauri kwamba mfumo huo pia utumike sio kutoa malaamiko tu, bali pia kupongeza kazi kubwa na muhumu inayofanya na FZS na wadau wengine kama Hifadhi ya Taifa Serengeti na wawekezaji walioko katika maeneo yao.
Mfumo wa Utaratibu wa Kutatua Matatizo umeanza kwa majaribio katika vijiji vyote tano; Robanda, Bokore, Bonchugu, Makundusi na Merenga.

Baada ya tathmini ya utekelezaji wake kukamilika na kujiridhisha na matokeo, FZS Tanzania inapanga kuusambaza mfumo huo katika maeneo mengine ya miradi yake, ikiwemo iliyopo katika wilaya zilizozunguka Ikologia ya Hifadhi za Taifa Serengeti, Katavi Mahale na Nyerere Selous.

Katika majadiliano yote ya vijiji vitano, watoa mada na washiriki walisisitiza kwamba makundi maalum, vijana, wanawake, wazee, walemavu na yatima ndiyo yanayobeba uzito mkubwa katika uhalisia wa maisha ya Serengeti, na hivyo hayawezi kuachwa nyuma katika mchakato wa kuimarisha mfumo wa kupokea na kutatua malalamiko.

Wawakilishi wa Halmashauri za Vijiji pamoja na viongozi wa vijiji walibainisha kwamba makundi hayo mara nyingi ndiyo hukumbwa na madhara ya moja kwa moja ya mabadiliko ya kimazingira, mashambulizi ya wanyama wakali, upotevu wa kipato, kukosa taarifa sahihi na changamoto za kushiriki kwenye maamuzi ya kijamii.

Hivyo, waliomba mfumo huo uweke njia mahsusi na nyeti za kuwafikia, ikiwemo kuwapa elimu kupitia mikutano ya hadhara, kutumia mabalozi wa kijamii kuwafikia walemavu na wazee, kuweka maeneo salama ya kutolea taarifa bila hofu ya kulipiziwa kisasi na kuhakikisha taarifa zinawafikia kwa lugha rahisi na kwa wakati.

Kwa kuzingatia maoni hayo, hatua inayofuata ya utekelezaji wa mfumo itahusisha kwenda moja kwa moja kwa makundi hayo na kuwapa nafasi ya kuelewa haki zao, namna ya kufikisha malalamiko yao na jinsi ya kupata mrejesho wa hatua zinazochukuliwa.

Lengo ni kuhakikisha kwamba mfumo huo hauwi wa viongozi pekee, bali ni mali ya kila mwanajamii, kuanzia mtoto anayekosa uwakilishi, kijana anayehitaji ajira na elimu ya uhifadhi, mwanamke ambaye sauti yake imekuwa ikipuuzwa, mzee anayehitaji heshima ya ushiriki, mlemavu anayehitaji msaada wa kufikia mikutano, hadi yatima ambaye mara nyingi hana pa kusemea.

Kwa kuwajumuisha katika hatua hiyo mpya, FZS inaweka msingi wa uhifadhi unaowahusisha watu wote na kuonesha kwamba miradi ya uhifadhi inabaki kuwa endelevu pale tu inapojengwa juu ya haki, ushirikishwaji na usawa wa makundi yote ya jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages