NEWS

Tuesday, 18 November 2025

Sifa zilizombeba Dkt. Nyansaho kuteuliwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa



Waziri mpya wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Simeon Nyansaho, akila kiapo mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dodoma, Novemba 18, 2025.

Na Mwandishi Wetu

Waziri mpya wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho, ni mfano wa mtu aliyebatizwa kwenye moto na kuibuka chuma cha pua.

Hakufika hapo kwa njia ya mkato, bali amepambana kila mahali alipopata fursa ya kufanya kazi. Silaha yake kubwa ni uchapa kazi na nidhamu ya kuwatumikia Watanzania.

Amekuwa alama ya uzalendo, juhudi, uadilifu na muumini anayethamini maisha ya watu wengine na mtu anayejiamini kwa kile anachokifanya.

Kitabia, Dkt. Nyansaho ni mnyenyekevu, muumini wa dhana ya kazí kama kipimo cha utu, na anakuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akitegemewa kuimarisha juhudi za pamoja katika kuiweka Tanzania salama ndani na nje ya mipaka yake.

Dkt. Nyansaho ni nani?
Msomi huyu wa masuala ya Uchumi na Biashara, hadi anateuliwa na Rais Samia kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Dkt. Nyansaho pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mwenyekiti wa Bodi ya Watumishi Housing Investments, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Azania.

Vyeo vingine ni Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Management Development for Health (MDH) na amewahi kuwa Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Azania.



Waziri mpya wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho.

Novemba 10, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Dkt. Nyansaho kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kabla ya kumteuwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Novemba 17, 2025.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages