
Na Christopher Gamaina
Tarime
------------
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Tarime, mkoani Mara kwa kushirikiana na Shirika la Plan International, imewaelimisha wakulima wa kahawa vijijini kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mbinu bora za kukabiliana nayo.
Wakulima hao kutoka vijiji vya Soroneta, Kemakorere, Muriba na Nyansincha wilayani Tarime walielimishwa umuhimu wa kupanda mazao ya muda mrefu, hasa miti rafiki wa mazingira ili kuongeza uhimilivu wa kilimo dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Mbali na elimu hiyo, waliwapata wazee wa kimila mafunzo kuhusu ufugaji wa nyuki na utunzaji wa mazingira ili kuwawezesha kujiongezea kipato huku wakilinda uendelevu wa rasilimali za misitu.
Aidha, kama sehemu ya utekelezaji wa programu hiyo, taasisi hizo zimegawa miche ya miti kwa wazee wa kimila kwa ajili ya msitu wao wa Binagi uliopo Mogabiri.
“Tumetekeleza shughuli hizo kati ya Machi na Julai 2025,” Askari wa Uhifadhi wa TFS Wilaya ya Tarime, Martin Ngongi, aliiambia Mara Online News mjini Tarime wiki iliyopita.
Alisema lengo ni kuimarisha hamasa ya jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uelewa wa wakulima kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu na mazingira kwa ustawi wa binadamu na uchumi endelevu.
No comments:
Post a Comment