NEWS

Sunday, 9 November 2025

Wananchi Serengeti wasubiri barabara ya lami Sanzate-Natta kwa shauku kuchochea uchumi



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati aliyevaa shati la drafuti), akizungumza na mkandarasi alipokwenda kukagua ujenzi wa barabara ya Sanzate- Natta, wilayani Serengeti wiki iliyopita.

Na Mwandishi Wetu
Akiripoti kutoka
Serengeti
---------------

Wakazi wa wilaya ya Serengeti na mkoa wa Mara kwa ujumla wanasubiri kwa shauku kubwa ukamilishaji wa barabara ya lami Sanzate- Natta (km 40) ili kuwasaidia kuharakisha maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.

Walitoa kauli hiyo Jumamosi iliyopita, wakati Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alipokwenda kukagua mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi China Railway Seventh Group Co. Ltd katika wilaya ya Serengeti yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori.

RC Mtambi alitaka mkandarasi huyo kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ambao ni sehemu ya barabara ya Makutano- Nyamuswa- Natta- Ikoma Gate (km 135) inayojengwa kwa kiwango cha lami kutokana na fedha za serikali.

“Serikali imetoa fedha, mkandarasi amerudi na tutaendelea kufuatilia,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa na kusisitiza umuhimu wa kazi za ujenzi wa barabara hiyo kuendelea bila kusimama.


RC Mtambi (aliyevaa shati la drafuti), akimwagiza mkandarasi kuharakisha ujenzi wa barabara ya Sanzate- Natta wiki iliyopita. Katikati aliyevaa miwani ni Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe.

Barabara ya Sanzate- Natta ni sehemu ya barabara ya lami inayotoka Musoma, Mara kuelekea mkoani Arusha kupitia hifadhi bora Afrika - Hifadhi ya Taifa Serengeti.

RC Mtambi alielekeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara kusimamia kwa karibu mradi huo ili kuhakikisha unatekelezwa kwa viwango na kukamilishwa kwa wakati uliopangwa.

“Hivi sasa mkandarasi anaendelea na kipande cha kilomita 8.4, kati ya hizo, kilomita 1.8 tumekwishaweka lami na imeishakamilika. Kwa hivyo, kwa sasa anadelea na kilometa 6.4,” Meneja wa TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe, alimweleza RC Mtambi.

Pia, katika taarifa yake hiyo, Mhandisi Maribe alibainisha kuwa hadi sasa mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 10.4 kati ya shilingi bilioni 51.7 zinazotarajiwa kugharimia ujenzi wa barabara ya Sanzate- Natta (km 40).

Kwa mujibu wa Meneja huyo TANROADS, kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefika asilimia 56 na kwamba unatarajiwa kukamilika Januari 2026.

Wakazi wa wilaya ya Serengeti wanaamini barabara hiyo ambayo itawaungunisha na mji wa Musoma kwa lami itakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwao.

“Barabara hii ikikamilika vipato vyetu vitaongezeka na hata gharama za usafiri zitapungua. Tunaishukuru serikali kwa kutoa fedha kuendeleza ujenzi wake maana imechukua muda mefu,” alisema mmoja wakazi wa Serengeti wanaoishi jirani na barabara hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco, alimshukuru RC Mtambi kwa kutembelea mradi huo uliokwama kwa muda mefu, akisema wananchi wana shauku ya kuona barabara hiyo ya lami inakamilika ili waanze kuitumia.

Ujenzi wa barabara hiyo ulianza Julai 2020 na ulitarajiwa kukamilika Julai 2022, lakini muda umekuwa ukiongezwa kutokana na sababu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages