NEWS

Tuesday, 2 December 2025

Barrick, Tarime DC waungana kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani 2025



Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye (aliyevaa fulana ya kijani), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Mgodi wa North Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Kampuni ya RIN kwenye maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Nyamongo, Desemba 1, 2025.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
----------

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara jana ulijumuika na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na wadau wengine kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu wa 2025, huku ukionesha unavyotumia mabilioni ya fedha kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kuboresha huduma za afya kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

Pia, mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals, ulifadhili maadhimisho hayo ambayo yalifanyika Nyamongo, jirani na mgodi huo.

Madhimisho hayo yaliwapa wananchi fursa ya kupata ushauri wa kitaalamu na huduma za afya, ikiwemo upimaji wa Virusi Vya UKIMWI (VVU) – zilizotolewa na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.


Wananchi wakipata ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya afya wakati wa maadhimisho hayo

"Kama mgodi, tumejitolea kuwa majirani na washirika wema, tukisaidia jitihada za kuboresha maisha na kuimarisha afya ya jamii. Mchango wetu kwenye sekta ya afya ni muhimu sana pamoja na ushiriki kwenye kampeni mbalimbali za afya kama hizi za upimaji wa VVU,” alisema Dkt. Nicholaus Mboya ambaye ni Meneja wa Idara ya Afya na Usalama katika Mgodi wa Barrick North Mara.

Dkt. Mboya alisema uwekezaji kwenye uelewa wa VVU na upimaji ni hatua muhimu katika kuzuia maambuizi mapya katika mapambano dhidi ya UKIMWI.


Dkt. Mboya akizungumza wakati wa maadhimisho hayo

Wadau wengine walioshikiri kufanikisha maadhimisho hayo ni ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Tarime na kampuni ya RIN ambayo ni moja ya wakandarasi wazawa wanaopata fursa za kibiashara katika mgodi wa Barrick North Mara.

Kwa mujibu wa Dkt. Mboya, Barrick imetumia takriban shilingi bilioni 5.4 sawa na asilimia 20 ya bajeti yake ya CSR katika mgodi wa North Mara kugharimia miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, nyumba za watumishi wa afya na ununuzi wa vifaa tiba tangu mwaka 2019 ilipochukua uendeshaji wa mgodi huo.

"Kwa mwaka huu wa 2025, kuna miradi ya afya ipatayo 21 yenye thamani ya Tsh. 2.4 bilioni. Miradi hii ipo katika hatua mbalimbali na mingi ikiwa imekamilika,” alidokeza Dkt. Mboya katika sehemu ya taarifa yake kwenye maadhimisho hayo.

Mmoja wa wazee akipokea kadi ya Bima ya Afya wakati wa maadhimisho hayo

Taarifa zilizotolewa katika maadhimisho hayo zinaonesha kushuka kwa maambukizi ya VVU katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kutoka asilimia 1.5 mwaka 2024 hadi 1.42 kufikia Novemba 2025.

Aidha, halmashauri hiyo imetumia maadhimisho hayo kuwapa wazee kadi za Bima ya Afya 2,000 ili kwawezesha kupata huduma za matibabu kwa urahisi.

Mpango huo wa kutoa kadi za Bima ya Afya ulifadhiliwa na mdau wa maendeleo na Mlezi wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Isack Charles Range, kupitia kampuni yake ya RIN Co. Ltd.


Mzee akikabidhiwa kadi ya Bima ya Afya wakati wa maadhimisho hayo

Akizungumza baada ya kukagua mabanda ya huduma mbalimbali za afya zilizotolewa wakati wa maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, Mwl. Sauli Mwaisenye, alitoa wito kwa jamii kujali malezi na matunzo mazuri kwa watoto ambao wazazi wao wamefariki dunia kutokana na UKIMWI.

“Watoto yatima ambao wamepoteza wazazi wao kutokana na jana la IKWMI watunzwe na kupatiwa haki zao za msingi,” DAS Mwaisenye ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele alisema.


DAS Mwaisenye (katikati) akikagua moja ya mabanda ya huduma za afya na ushauri katika maadhimisho hayo

DAS Mwaisenye alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweka mkakati wa kubaini vyanzo vya maambukizi mapya na kupima VVU, pamoja na kuzingatia suala la tohara salama kwa wanaume, miongoni mwa hatua nyingine.

Mbali na kupiga vita mambukizi ya VVU, wananchi waliohuduria maadhimisho hayo walisema husadia kuhamasisha jamii kuepukana na vitendo vya ukatilii wa kijinsia, hususan kwa watoto na wanawake.

“Maadhimisho haya ni chachu ya maendeleo katika maeneo yetu yanayozunguka mgodi wa North Mara maana husadia watu kujua hali za afya zao,” alisema mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Getango Petro.


Wazee wakiwa wamejipanga mstari kwa ajili ya kupokea kadi za Bima ya Afya kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakati wa maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani hufanyika Desemba 1 kila mwaka kutathmini mwenendo wa hali ya VVU ili kuimarisha mikakati ya kuzuia mambukizi mapya na kuwakumbuka watu waliokufa kutokana na janga hilo, miongoni mwa mambo mengine.

Kaulimbiu ya Siku ya UKIMWI Duniani Mwaka huu wa 2025 ni “Shinda Vishawishi, Imarisha Mwitiko, Tokomeza UKIMWI.”

Wakati huo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, jana alisema serikali itandelea kuboresha huduma kwa wenye VVU, ikiwemo kuwapa dawa za ARV za kufubaza viruzi hivyo bila malipo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages