NEWS

Wednesday, 29 April 2026

Mamia wanufaika na mikopo ya bilioni 3.5/- ya asilimia 10 Halmashauri ya Wilaya ya Tarime



Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara (katikati), akiwa kwenye pikipiki na baadhi ya vijana waliopata mikopo ya asilimia 10 katika jimmbo hilo, hivi karibuni.

Na Mwandishi Maalumu
---------------------------------

Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara imeendelea kutekeleza kwa vitendo utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Halmashauri hiyo imeweza kutoa mikopo ya shilingi takriban bilioni 3.5 kwa vikundi 395 vya makundi hayo ya jamii katika kipindi cha mwaka 2024/2025 na mwaka 2025/2026.

Mikopo hiyo ambayo hutolewa bila riba inalenga kuwawezesha wananchi hao kiuchumi na hivyo kuboresha hali yao ya maisha.

“Mikopo hii imesaidia kuinua hali ya uchumi kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika halmshauri yetu ya wilaya ya Tarime,” Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Anthony George aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara katika mahojiano maalum ofisini kwake, hivi karibuni.

Alisema kuwa mikopo hiyo imetengeneza ajira kwa makundi hayo na hivyo kuyawezesha kuondokana na hali ya umaskini na utegemezi katika jamii.

“Mikopo hii imesaidia kupunguza utegemezi kwa wanaufaika,” alisema afisa huyo wa serikali.

Nyange alisema manufaa yanayotokana na mikopo hiyo kwa sasa yamekuwa chachu kwa wengi kujitokeza kuchangamkia mikopo hiyo ya asilimia 10 katika halmashauri hiyo tofauti na kipindi cha nyuma.

Mapema mwezi huu, halmashauri hiyo ilikabidhi pikipiki kadhaa ikiwa sehemu ya mikopo hiyo ya asilimia 10 kwa kwa vijana kwa ajili ya biashara ya kubeba abiria.

Makabidhiano ya pikipiki hizo yalishuhudiwa na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijii, Mwita Waitara, miongoni mwa viongozi wengine katika ofisi za halmashauri hiyo zilizopo kata ya Nyamwaga.

“Vijana wengi wamependelea biashasra ya bodaboda… bodaboda kama 250 zimeingia barabarani kufanya biashara,” alisema Nyange.

Alisema biashara ya bodaboda inaonekana kushamiri kutokana na jiografia ya maeneo mengi, yakiwemo ya wachimbaji wadogo wa madini na masoko ambapo pikipiki hupita kwa urahisi na hivyo kuifanya hiyo biashara kulipa kwa vijana.

Habari njema ni kwamba urejeshaji wa mikopo ni mzuri, jambo ambalo litatoa fursa kwa vikundi vingi zaidi kuendelea kunufaika na mikopo hiyo ya asilimia 10.

“Hali ya urejeshwaji wa mikopo hii ya asilimia 10 katika halmashauri yetu ni nzuri,” alisema Nyange.

Halmashauri hiyo pia imekuwa ikitoa mafunzo maalum ya kuvijengea uwezo vikundi hivyo ili kuviwezesha kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa miradi ya kiuchumi.

Mafunzo hayo yanahusisha mada mabalimbali kama vile uwekaji wa akiba, uwekezaji, marejesho ya mkopo, usimamizi wa fedha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Inaelezwa kuwa halmashauri hiyo ambayo imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali mabalimbali, ikiwemo madini, inaongoza kwa kutoa kiasi kikubwa cha mikopo ya asilimia 10 katika mkoa wa Mara.

Mbali na kutoa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pia imekuwa ikishirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kutoa ruzuku ya fedha kuwezesha vikundi vya vijana kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Tayari kiasi cha shilingi milioni 220 kutoka mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) wa mgodi huo zimetolewa kuwezesha vikundi 13 vya vijana kuanzisha miradi ya kiuchumi katika vijiji vyote 11 vinavyouzunguka.

Tayari vikundi hivyo vilishapokea fedha hizo, ikiwa ni ruzuku ya CSR ya mwaka uliopita kutoka mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Kwa mujibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, fedha hizo zimesaidia vijana takriban 100 wanachama wa vikundi hiyo kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages