NEWS

Saturday, 13 December 2025

Halmashauri Kuu CCM Mara yakutana kutathmini Uchaguzi Mkuu 2025 mkoani humo

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (katikati waliokaa), akiongoza kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara, wilayani Serengeti jana.

Na Mwandishi Wetu
Serengeti
-------------

Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara imekutana kutathmini na kujadili mafanikio ya Uchaguzi Mkuu uliopita, na namna chama hicho tawala kinapaswa kuisimamia serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Kikao hicho kilifanyika wilayani Serengeti, Ijumaa, Desemba 12, 2025, kikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi.

Pamoja na tathmini ya Uchaguzi Mkuu uliopita, Mwenyekiti Chandi aliweka msisitizo wa kuimarisha amani, utulivu na mshikamano kama nguzo muhimu za maendeleo endelevu kwa mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla.

Alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ushindi mkubwa aliopata kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, na namna anavyozidi kuonesha nia ya dhati ya kuiongoza Taifa. 

Pia, aliwapongeza wenyeviti wa wilaya na viongozi wote wa CCM mkoani Mara kwa uchapa kazi uliokiwezesha chama hicho kupata ushindi wa kishindo kwenye Uchaguzi Mkuu.

Mwenyekiti Chandi akizungumza katika kikao hicho

"Niwashukuru wenyeviti wa CCM pamoja na viongozi mbalimbali, mnafanya kazi kubwa sana, kwa ushindi aliopata Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan - asilimia 98, mmeheshimisha mkoa wa Mara.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Iddi Mkowa, alisema: "Ushindi huo mkubwa unaonesha ni jinsi gani Watanzania wanamkubali Dkt. Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi (CCM)."

Katika hatua nyingine, Chandi aliwapongeza wenyeviti wa halmashauri waliochaguliwa hivi karibuni na kuwataka kusimamia ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato ya halmashauri zao.

"Wenyeviti wa halmashauri, hongera kwa ushindi mlioupata, ili muwe na nguvu lazima msimamie halmashauri zenu kwa kukusanya mapato na kuanzisha vyanzo vipya kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” alisema.

Kwa upande mwingine, Chandi aliwataka wabunge kuhakikisha wanawaunganisha wanachama kwa kuvunja makundi ndani ya CCM, pamoja na kufanya mikutano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yao ya uongozi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha, alisema: "Tunaungana na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kila kona ya nchi kama ilivyo dhamira yake.”

"Kwa mikono miwili tumeipokea kauli ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa - kuhakikisha tunaenda kufanya kazi kwa bidii kwa kukusanya mapato kwa vyanzo vilivyopo na kuanzisha vipya ili kupata fedha za kupeleka maendeleo kwa wananchi,” aliongeza Matera.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages