NEWS

Monday, 15 December 2025

Matokeo mabaya Darasa la Saba 2025 Mara: RC Mtambi awaweka 'kiti moto' Ma-DC, awapa siku 7 kutoa maelezo



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
-------------

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Alfred Mtambi, ametoa siku saba kwa Wakuu wa Wilaya za mkoa huo kutoa maelezo ya sababu za ufaulu usioridhisha katika matokeo ya Mhitani wa Taifa wa Darasa la Saba Mwaka 2025.

Mtambi alitoa agizo hilo wiki iliyopita mjini Musoma katika kikao cha kujadili masuala ya elimu, baada ya kupokea taarifa ya matokeo ya mtihani huo ya mkoa wa Mara, ambayo yalionesha kuporomoka kwa ufaulu.

“Ninatoa siku saba kwa Wakuu wa Wilaya nipate maelezo ya sababu za ufaulu usioridhisha katika wilaya zenu na namna zilivyojipanga kuboresha ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2026,” alisema.

Alisisitiza kuwa ufaulu wa darasa la saba mwaka 2025 kwa mkoa wa Mara hauridhishi na kuwataka viongozi wa wilaya na halmashauri kubainisha sababu za ufaulu duni ili hatua stahiki zichukuliwe haraka.

Kikao hicho pia kilijadili mikakati ya kuinua ufaulu kwa mwaka 2026, ambayo ilitolewa na Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Kuhusu mapokezi ya wanafunzi wapya shule za awali, msingi na kidato cha kwanza mwakani, Mtambi alizitaka halmashauri zote kuhakikisha zinakamilisha maandalizi, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wazazi kuandikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule.

Aliziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kukamilisha kwa wakati ujenzi wa shule mpya, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo ya shule za msingi zilizopokea fedha zilizotolewa kupitia Mradi wa BOOST ili shule zinapofungua kuwe na miundombinu ya kutosha.

Wakati huo huo, Mkuu huyo wa mkoa ameziagiza halmashauri kuongeza juhudi katika usimamizi wa makusanyo ya mapato ya ndani na kuboresha usafi wa mazingira, hususan maeneo ya pembezoni mwa barabara, shule, masoko na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu.

Awali, akitoa taarifa hiyo, Mwakilishi wa Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu, Kinyemi Sepeku, alisema shule 905 za mkoa huo zilisajili watahiniwa wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi Mwaka 2025.

Sepeku alibainisha kuwa wanafunzi 64,940 walisajiliwa kufanya mtihani huo, kati yao, 62,589 sawa na asilimia 96.4 ya wanafunzi wote waliosajiliwa walifanya mtihani huo, huku wanafunzi 2,351 hawakuhudhuria kutokana na sababu mbalimbali.

“Wanafunzi waliofaulu ni 42,226 sawa na asilimia 67 ya wanafunzi wote waliofanya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba Mwaka 2025 katika mkoa wa Mara,” alisema na kuongeza kuwa wanafunzi 20,369 sawa na asilimia 33 ya waliofanya mtihani huo wamefeli.

Katika matokeo ya mtihani huo, Sepeku alisema Halmashauri iliyofanya vizuri ni ya Mji wa Tarime ikifuatiwa na Manispaa ya Musoma, huku halmashauri za wilaya za Bunda na Musoma zikiwa zimefanya vibaya zaidi katika ngazi ya mkoa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages