
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir.
Mwanza
------------
Serikali itaongeza udahili wa wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza kutoka 358 hadi 2,000, imeelezwa.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, hatua hiyo ni moja ya mbinu za kuimarisha uwezo wa kampasi hiyo ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Naibu Waziri Wanu aliyasema hayo jijini Mwanza Jumapili, Desemba 14, 2025 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano Afrika Mashariki (EASTRIP) wa DIT.
Alimtaka mkandarasi COKGIX & ENGINEERING anayetekeleza mradi huo kuongeza kasi ili kuukamilisha kwa wakati kulingana na mkataba wake.
Pia, aliwataka wazabuni wote kuhakikisha mitambo na vifaa vya mradi huo vinawasili na kufungwa kwa wakati ili kuwezesha utoaji wa mafunzo kwa wakati.
Alisema ucheleweshaji wa ujenzi unaweza kuathiri malengo ya serikali ya kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na umahiri unaohitajika katika soko la ajira la ndani na kimataifa, kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri Wanu liwahakikishia wananchi na uongozi wa DIT kuwa serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa kampasi hiyo, ikiwemo kuongeza udahili wa wanafunzi.
Kampasi ya DIT ya Mwanza ni mahali panapojengwa Kituo cha Kanda cha Umahiri cha Uchakataji na Utengenezaji wa bidhaa za Ngozi.
Mradi huo, kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, unahusisha majengo ya kufundushia, taaluma, hosteli mbili na karakana kwa ajili ya mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi.
Prof. Mushi alisema ujenzi wa majengo hayo unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ambayo imetoa mkopo wa riba nafuu kufanikisha mradi huo kwa gharama ya shilingi bilioni 37.
Mkurugenzi wa DIT Kampasi ya Mwanza, Dkt. John Msumba, alisema taasisi yake imefufua sekta ambayo ilikuwa imekufa kwa kukosa wataalamu, na kwamba kwa sasa viwanda vya ndani vinapata wataalamu - tofauti na awali ambapo ililazimu kuwatoa nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment