NEWS

Tuesday, 2 December 2025

Mwenyekiti mpya, Makamu wake Halmashauri ya Wilaya Tarime waahidi kuchapa kazi



Makamu Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Juster Magabe, akizungumza katika Baraza la Madiwani, Nyamwaga, jana Desemba 2, 2025. Wanaomfuatia ni Mwenyekiti mpya wa Halmashauri, Matera Chacha, Mkurugenzi Mtendaji, Solomon Shati na DAS Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
----------

Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha na Makamu wake, Juster Daudi Magabe, wamesisitiza ushirikiano na kuchapa kazi, kwa maslahi mapana ya wananchi.

"Nitoe shukrani kwa madiwani kwa kuniamini na kufanya maamuzi haya, uchaguzi umeisha, nawaombeni tushirikiane tufanye kazi tuliyotumwa, tushirikiane na watumishi kuhakikisha halmashauri inasonga mbele.

"Sasa ni muda wa kufanya kazi, twende tukatekeleze zile ahadi tulizoahidi wananchi, hatuna muda wa kupoteza,” alisema Matera baada ya kutangazwa mshindi katika kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika Nyamwaga, jana Desemba 2, 2025.

Naye mshindi wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti mpya wa halmashauri hiyo, Juster, alisema: "Nishukuru sana madiwani wenzangu kuniamini, ninawaahidi ushirikiano, nitamshauri vyema mwenyekiti wetu, nitalinda maslahi ya madiwani na nitafikika kwa urahisi.”

Aliongeza: "Kikubwa twendeni tukachape kazi, uchaguzi umeisha, lazima maisha mengine yaendelee, kikubwa kwetu ni maendeleo na kuwawakilisha vyema wananchi wa kata zetu.”

Uchaguzi wa viongozi hao; Matera (Diwani wa Kata ya Manga) na Juster (Diwani wa Kata ya Nyakonga), ulisimamiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye.

Kikao hicho cha Baraza la Madiwani kilihudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Solomon Shati, miongoni mwa viongozi wengine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages