
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akiambatana na Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Mboni Mhita, katika ziara ya kukagua kongani ya uwekezaji ya Buzwagi (Buzwagi Special Economic Zone).
Na Mwandishi Wetu
Buzwagi
------------
Viwanda zaidi ya 30 vitajengwa katika kongani ya Buzwagi wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, serikali imeeleza.
Mpaka sasa tayari mwekezaji East Africa Conveyors Supplies ameanza uzalishaji wa bidhaa za migodini katika kongani hiyo.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema shabaha ya kuanzishwa kwa kongani ya viwanda ni kuwanufsisha wananchi wa Kahama na taifa kwa ujumla kupitia ajira na shughuli nyingine.
Waziri Mavunde aliyasema hayo baada ya kutembelea eneo hilo la Buzwagi, Jumapili Desemba 21, 2025.
Alisema viwanda vitakavyojengwa vitajihusisha na sekta mbalimbali zikiwemo nishati, elimu, uzalishaji wa bidhaa za migodini na vipuli vya viwanda.
"Hii ni hatua muhimu sana kwenye sekta ya madini kwa sababu bidhaa hizo zilikuwa zikiagizwa nje," alisema Mavunde.
Waziri huyo alidokeza kuwa Kampuni ya Tembo Nickel itajenga kiwanda cha kuongeza thamani madini ya metali (Multi-Metál Refinery Facility) katika eneo hilo la kongani.
Kiwanda hicho kitakuwa moja ya viwanda vikubwa barani Afrika ambacho kitatumia teknolojia ya kisasa iitwayo "hydromet" ambayo inatumia umeme kidogo badala ya kuyeyusha kwa joto kali.
Akizungumza baada ya matembezi katika kongani hiyo ya Buzwagi, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, alisema eneo hilo lina miundombinu mizuri, umeme na vyanzo vya majà kwa ajili ya Watanzania kuchangamkia uwekezaji.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania, Glead Teri, alisema serikali kwa kushirikiana na wawekezaji imeanzisha Buzwagi Special Economic Zone kuwa kitovu cha uzalishaji, usindikaji na usambazaji wa bidhaa za mgodi kwa soko la Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.
No comments:
Post a Comment