
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Chacha (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, kwenye mkutano wa hadhara katani Manga, jana.
Tarime
----------
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Chacha na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, wameahidi kushirikiana kuchapa kazi na kuhamasisha mshikamano wa koo zote katika halmashauri hiyo.
Viongozi hao wa wananchi waliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katani Manga, Jumapili Desemba 7, 2025.

Mkutano huo uliandaliwa na Mwenyekiti Matera kuwashukuru wakazi wa kata hiyo kwa kumuamini na kumchagua kuwa diwani wao kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
"Ninatoa shukrani kwenu wananchi, nilipenda kujumuika nanyi kwa lengo la kuwashukuru, mmeniunga mkono kwa kila hali na hatimaye nimekuwa diwani wenu, na sasa hivi mimi ni Mwenyekiti wa Halmashauri yetu," alisema.

Mwenyekiti Matera akizungumza katika mkutano huo
"Nakwenda kuchapa kazi kwa kutenda haki kwa kata zote 26, vijiji 88 na vitongoji 500. Sitawaangusha, nitahakikisha kila kata inapata huduma za jamii, ikiwemo maji, barabara, afya na umeme bila ubaguzi, nakwenda kusimamia watu wapate maendeleo.
"Nitahakikisha ‘keki’ ya halmashauri inagawanyika sawa bila upendeleo, endeleeni kuni- suport hadi matunda yaonekane,” alisema Mwenyekiti Matera.

Kwa upande wake Mbunge Waitara aliahidi kumpa Mwenyekiti Matera ushirikiano wa dhati katika kushughulikia maendeleo ya wananchi.
"Tutashikana mkono ili tuweze kuleta maendeleo katika jimbo la Tarime Vijijini, tujitahidi kuunganisha koo za Wakurya kwa kumtendea kila mtu haki, sitaki kusutwa kwa kumuonea mtu.
"Nawashauri vijana msishiriki maandamano, kama kuna changamoto tuzungumze kupitia wenyeviti wa vijiji, mbunge na madiwani, badala ya vurugu,” alisisitiza mbunge huyo.

Mbunge Waitara akisisitiza jambo kwenye mkutano huo
Naye mgeni rasmi katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliwahakikishia wananchi kuwa wilaya iko salama, hivyo waendelee na shughuli zao bila hofu yoyote.
"Tarime iko Salama, mpo salama, tumejipanga vizuri, tumeimarisha usalama kila kona, tumemiliki anga na ardhi, msiwe na mashaka - fanyeni kazi zenu msiwe na mashaka,” alisema na kuendelea:
"Wanaolima walime, wanaochimba wachimbe, wanaohamasisha hayo maandamano wana malengo yao - wamechungulia utajiri na amani tuliyo nayo inawauma, wanachotaka watuharibie, huo ni wivu.”

DC Gowele akiwahakikishia wananchi usalama
Wananchi wakicheza ngoma ya asili katika mkutano huo

No comments:
Post a Comment