NEWS

Friday, 16 January 2026

Nyambari Nyangwine atuma salamu za pole kifo cha Macheda, aungana na wakazi wa Tarime kuomboleza



Nyambari Nyangwine

Na Mwandishi Wetu

Mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangiwne, ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha Wambura Kisike maarufu kwa jina la Macheda, mkazi wa mji wa Tarime mkoani Mara.

“Nimeshitushwa sana na kifo cha huyu kijana Macheda, na naungana na wakazi wa Tarime katika kipindi hiki cha kuondokewa na mpendwa wetu,” Nyangwine ameiambia Mara Online News kwa simu akiwa nje ya nchi.

Nyambari ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime kupitia chama tawala – CCM, ametoa pole pia kwa familia ya marehemu Macheda.


Macheda enzi za uhai

Taarifa za kifo cha Machdeda ambaye alikuwa fundi umeme na kada wa CCM, zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana Alhamisi mchana, baada ya kudaiwa kujinyonga chumbani kwake katika mtaa wa Nkende.

Wakazi wa Tarime wameeleza kushitushwa na kifo hicho wakimuelezea Macheda kama kijana aliyekuwa mstari wa mbele katika kushiriki shughuli za kijamii na mwenye upendo kwa watu.

Mwili wa Macheda unasafirishwa leo kwenda nyumbani kwao jijini Mwanza kwa ajili ya mazishi.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages