Afisa wa DCEA Kanda ya Ziwa, Dezidel Tumbu. akiwasilisha mada kwa watumishi wa kituo cha forodha katika mpaka wa Sirari wilayani Tarime leo.
Tarime
-----------
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewapa watumishi wa kituo cha forodha cha mpaka wa Sirari wilayani Tarime elimu kuhusu dawa hizo.
DCEA imetoa elimu hiyo leo Jumatano, Januari 7, 2026 kwa lengo la kuwajengea watumishi hao uwezo wa kujua madhara, kufuatilia, kudhibiti na kupambana na uingizwaji wa dawa za kulevya nchini kupitia njia ‘bubu’ mpakani hapo.

Sehemu ya watumishi wakifuatilia mada

Afisa wa DCEA Kanda ya Ziwa, Dezidel Tumbu, akigawa vipeperushi wakati wa utoaji wa elimu hiyo.
"Kwa elimu hii, wafanyakazi wa kituo jumuishi cha Sirari wameelewa madhara yatokanayo na dawa kulevya kwamba yanapoingia nchini hupoteza nguvukazi ya Taifa,” amesema Tumbu.
Ameongeza: "Mwitikio wa watumishi umekuwa ni mkubwa, tunamshukuru Kamishna Jenerali [wa DCEA] kuruhusu kuja kutoa elimu hii, wameahidi watakuwa sehemu ya mapambano ya dawa za kulevya hapa [Sirari].”

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii kutoka DCEA Kanda ya Ziwa, Ester Malinya, amesema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa watu wengi wamekuwa wakienda hospitalini kutafuta tiba ya afya ya akili kutokana na kuathiriwa na dawa za kulevya.

Ester Malinya akiwasilisha kwa watumishi hao mada kuhusu madhara ya dawa za kulevya

Ester akionesha mifano ya dawa za kulevya
Kaimu Afisa Mfawidhi Kituo cha Forodha Sirari, Emmanuel Mchunguzi, amekiri kuwa elimu waliyoipata imewapa mwanga wa kusaidia kupambana na dawa za kulevya.
"Elimu hii ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwetu familia ya wanaforodha imetupa mwanga na kutuongezea ufahamu zaidi katika kupambana na kudhibiti dawa za kulevya zisiweze kuingia nchini, tunashukuru sana.
"Watumishi wa umma ni sehemu ya jukumu letu kuhakikisha kuwa bidhaa hizi zote ambazo tumefundishwa zinazohusiana na dawa za kulevya tunazidhibiti pamoja na kuwasiliana na DCEA ili kuchukua hatua zaidi za kisheria,” amesema Mchunguzi.

Mchunguzi akieleza mbinu zinazotumiwa na wauzaji wa dawa za kulevya
Naye Mrakibu Mwandamizi, Afisa Mfawidhi Kituo cha Uhamiaji Sirari, Idd Jumbe Yahaya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mpaka wa Sirari amesema elimu hiyo imewakumbusha wajibu wa kupambana na dawa za kulevya.
"Elimu hii ina faida, imekuja kutukumbusha kuwa sisi ni sehemu ya wasimamizi wa kuzuia dawa za kulevya. Kila mtumishi ameona ana wajibu wa kudhibiti dawa za kulevya,” amesema Yahaya.
No comments:
Post a Comment