
Mkurugenzi wa Kemanyanki Contractors Manpower and Supply Company Ltd, Nicolaus Mahando Mgaya "Chichache".
Tarime
-------------
Kemanyanki Contractors Manpower and Supply Company Ltd inakwenda kuandika historia nyingine Jumamosi Januari 31, 2026 itakaposherehekea Maadhimisho ya Saba ya Siku yake, yaani Kemanyanki Day.
Maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya Chichake Sports Bar & Grill iliyopo Nyamongo, wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Pamoja na matukio mengine, Kemanyaki itatumia fursa hiyo kuelezea mafanikio lukuki iliyopata hadi sasa na dira ya baadaye ya kampuni hiyo ya wazawa ambayo inakua kwa kasi na kuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya ujenzi na huduma za mgodini.
Lakini pia, imeandaa zawadi mbalimbali kwa ajili ya wafanyakazi waliofanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao kazini, ambazo watakabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ambaye atakuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo.
Tangu ianzishwe, Kemanyanki Contractors imejipambanua kwa mchango wake mkubwa kwa jamii inayouzunguka mgodi wa North Mara, hasa kupitia ajira kwa wakazi wa eneo hilo, wengi wao wakiwa vijana.
Kupitia sera yake ya kutoa kipaumbele kwa rasilimali watu wa ndani, kampuni hiyo imechangia kupunguza ukosefu wa ajira, kukuza ujuzi na kuinua maisha ya familia nyingi katika jamii husika.
Hata hivyo, huwezi kuelezea mafanikio ya Kampuni ya Kemanyanki bila kutaja Kampuni ya Barrick inayoendesha Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
“Tunaishukuru sana Kampuni ya Barrick kwa kutengeneza fursa endelevu za kunufaisha jamii inayozunguka mgodi wa North Mara,” anasema Mkurugenzi wa Kemanyanki Contractors Manpower and Supply Company Ltd, Nicolaus Mahando Mgaya - maarufu kwa jina la Chichache.
Ushirikiano unaotolewa na mgodi huo unatajwa kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya kampuni hiyo na maendeleo ya jamii, ukidhihirisha namna sekta binafsi na wadau wa maendeleo wanavyoweza kushirikiana kwa manufaa ya wote.
“Tumekuwa na mafanikio makubwa kutokana na mchango mkubwa tunaopata kutoka Kampuni ya Barrick,” alisisitiza Chichake katika mahojiano maalum jana Jumatano huku akitaja baadhi ya mafanikio hayo.
“Mwaka 2025 tulifanya kazi bila kupata ajali yoyote ile - wafanyakazi wetu wote walitoka kwenda kazini na kurudi nyumbani salama,” alisema na kuweka wazi kuwa wafanyakazi 624 wamenufaika na Kemanyanki Contractors kati ya mwaka 2023 na 2025.
Alibainisha kuwa asilimia 90 ya ajira walizotoa ziligusa wazawa kutoka vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara na kwamba asilimia 80 ya wafanyakazi hao ni vijana.
“Wafanyakazi wetu waliokuwa na hali duni sasa hivi asilimia 70 ya hao wamejenga makazi ya kudumu, na tunawapa motisha ya kuwakopesha vifaa vya ujenzi bila riba,” alisema Mkurugenzi Chichake.
Aidha, alisema elimu ya ujasiriamali wanayowapa wafanyakazi wa kampuni hiyo na jamii inayozunguka mgodi wa North Mara imewasaidia wengi wao kuanzisha shughuli zao binafsi za kuwaingizia kipato.
“Tumekutanisha wanavijiji na viongozi wa mgodi ili kuelimisha jamii faida za mgodi huu. Tumesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la vijana wanaovamia mgodi, na jamii sasa imekuwa sehemu ya ulinzi wa mgodi,” alisema Chichake.
Kwa upande mwingine, alisema Kampuni ya Kemanyaki Contractors imekuwa ikitoa misaada ya kuchangia vifaa vya shule vikiwemo vya michezo kwenye shule zenye uhitaji, pamoja na kuwezesha baadhi ya wafanyakazi wake kukabili mahitaji ya elimu, hususan ada na michango ya shule.
“Vilevile, tumekuwa tukitoa ufadhili wa kuwalipa walimu wa masomo ya sayansi katika shule zenye upungufu wa walimu hao,” aliongeza Chichake.
Mkurugenzi huyo wa Kemanyanki Contractors Manpower and Supply Company Ltd alihitimisha kwa kuwaomba waalikwa wote kuhudhuria sherehe hiyo ya Kemanyanki Day, wakiwemo viongozi wote wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment