Mmoja wa wakazi wa Tarime akiwasilisha malalamiko yake mbele ya Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29 leo.
Tarime
----------
Wakazi wa wilaya ya Tarime mkoani Mara wamejitokeza kwa wingi kuwasilisha malalamiko na maoni yao mbele ya Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime leo Ijumaa, Januari 9, 2026 mbele ya wajumbe wa Tume hiyo, Balozi David Joseph Kapya na Balozi Radhia Naima Msuya.
Wajumbe wa Tume hiyo wakipokea malalamiko ya wakazi wa Tarime
Wananchi mbalimbali – wanawake kwa wanaume wamepata nafasi ya kueleza walivyoathiriwa na vurugu za Uchaguzi Mkuu, ikiwemo kuuawa, kupotea na kuumizwa kwa ndugu zao.
Baadhi yao, hasa wanawake wameshindwa kujizuia kulia na kububujikwa machozi wakati wakieleza machungu na magumu wanayopitia baada ya kuuawa na kupotea kwa waume na watoto wao waliokuwa wakiwategemesha kimaisha.
Wamelalamikia pia kunyimwa ushirikiano kwenye vyombo vya dola, hususan ofisi zenye dhamana ya ulinzi wa usalama wa raia na mali zao wakati wakifuatilia ndugu zao waliouawa na kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Sambamba na hayo, waathirika waliopata ulemavu wa viungo vya mwili walitumia nafasi hiyo pia kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia msaada wa viungo bandia.
Mwananchi mwingine akiwasilisha malalamiko yake
Kwa upande wa utoaji maoni, baadhi ya wananchi wamedai kuwa chanzo cha vurugu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu ni malimbikizo ya matatizo ya wananchi na vitendo vya rushwa hadi kwenye chaguzi za kisiasa.
Hata hivyo, katika tukio ambalo halikutarajiwa, umati wa wananchi uliokuwa ukionekana na nyuso za huzuni na majonzi ukumbini, ulilipuka kwa kumpigia makofi ya nguvu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye “Namba Tatu”, kwa maoni aliyowasilisha kwa Tume hiyo.
Namba Tatu ambaye alianza kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuunda Tume hiyo ya uchunguzi, amedai kuwa chanzo kikuu cha vurugu zilizotokea ni kukatwa kwa majina ya wawania ubunge walioshinda katika kura za maoni ndani ya CCM.
Alitaja sababu nyingine ya maandamano na vurugu za Uchaguzi Mkuu uliopita kuwa ni baadhi ya wasaidizi wa Rais, wakiwemo viongozi wa chama tawala – CCM kutokuwa karibu na wananchi wa chini ili kusikiliza na kuwasaidia kutatua shida zao.
“Viongozi wa chama tawala wawe karibu na wananchi – wasikilize shida zao,” amesisitiza Namba Tatu akiwa amevaa suti ya rangi ya kijivu na nembo ya picha ya Rais Samia.
Namba Tatu akiwasilisha maoni yake mbele ya Tume ya Rais ya uchunguzi
Baada ya kupokea malalamiko na maoni ya wananchi hao wa Tarime, Mwenyekiti wa mkutano huo, Mjumbe wa Tume ya Uchunguzi, Balozi Kapya, aliahirisha mkutano.
Balozi Kapya na Balozi Radhia wanatarajiwa kuwa na mkutano wa Tume hiyo wa kupokea malalamiko na maoni ya wakazi wa wilaya ya Bunda kesho Jumamosi, Januari 10, 2026.
No comments:
Post a Comment