NEWS

Monday, 5 January 2026

Morocco ilivyozima safari ya kihistoria ya Tanzania AFCON 2025




Ndoto ya Tanzania kuendelea kuandika historia mpya katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 imefikia tamati katika jiji la Rabat, baada ya Taifa Stars kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika mchezo wa raundi ya 16 bora.

Ilikuwa ni mechi iliyobeba hisia nyingi, matumaini makubwa, na jaribio la mwisho la kuvuka mpaka wa kihistoria ambao soka la Tanzania halijawahi kuuvuka.

Katika uwanja wa Prince Moulay Abdellah, Januari 4, 2026, Tanzania haikuingia kama timu iliyokuja kujitetea au kusubiri kipigo. Badala yake, iliingia ikiwa na ujasiri, nidhamu na mpango wa wazi wa kupambana na moja ya timu bora zaidi barani Afrika.

Kwa muda mrefu wa mchezo, Taifa Stars waliweza kuhimili presha ya wenyeji na hata kuifanya Morocco ionekane timu ya inayohaha kuliko ilivyotarajiwa.

Hata hivyo, kama ilivyo kawaida katika michezo mikubwa, tofauti ilijitokeza katika eneo dogo lakini muhimu zaidi, matumizi ya nafasi.

Tanzania ilipata nafasi ambazo zingeweza kubadili kabisa mwelekeo wa mchezo, lakini ukosefu wa umakini wa mwisho uliwagharmu kwa gharama kubwa dhidi ya timu yenye ubora wa hali ya juu.

Mwisho wa dakika 90, Morocco waliondoka wakiwa na tiketi ya robo fainali, huku Tanzania ikibaki na maswali, mafunzo na heshima. Ingawa safari ya kihistoria ya Taifa Stars imeishia hapa, namna walivyocheza na walipofikia, imeacha ujumbe mzito kwa Afrika nzima kuhusu mwelekeo mpya wa soka la Tanzania.

Mchezo huu utabaki kukumbukwa kama moja ya mechi ambazo Tanzania ilikuwa karibu zaidi kuliko wakati wowote kushinda mechi ya AFCON.

Katika kipindi cha kwanza na mapema kipindi cha pili, Taifa Stars walipata nafasi mbili za wazi ambazo zingeweza kubadili historia yao katika mashindano haya. Feisal Salum 'Fei Toto' na Simon Msuva walijikuta uso kwa uso na lango la Morocco, lakini maamuzi ya haraka na umakini wa mwisho vilikosekana. Haya ni matukio mawili hawatayasahau, ukiacha tukio la tatu la goli waliloruhusu la Diaz. Huenda kukosa nafasi hizo kuliathiri mchezo kisaikolojia.

Kadri dakika zilivyosonga mbele, presha ilianza kuongezeka kwa Tanzania huku Morocco wakizidi kujiamini taratibu. Hii ni hali ambayo imekuwa ikijirudia mara nyingi kwa Taifa Stars katika mashindano makubwa, kutengeneza nafasi, lakini kushindwa kuzitumia.

Dakika ya 90, tukio la kuangushwa kwa Iddy Nado kwenye eneo la hatari, bechi lote la ufundi na wachezaji wote wa Tanzania wakiwemo wachezaji wa akiba walilalamika kunyimwa penati. Mwamuzi wa mchezo hakuruhusu kutizamwa kwa VAR, jambo lililolalamikiwa na Taifa Stars.

Katika mechi za aina hii, hasa dhidi ya timu zenye uzoefu mkubwa wa kimataifa, kosa moja au nafasi moja iliyopotea inaweza kuamua hatima ya timu. Morocco hawakuhitaji nafasi nyingi, lakini Tanzania ilihitaji zaidi ya nafasi walizopata, walihitaji umakini wa kiwango cha juu ambao bado ni changamoto kwa soka la Tanzania katika hatua kubwa kama hizi.

Kukosa huku kumeendeleza rekodi ngumu ya Tanzania katika michuano ya AFCON, ambapo bado hawajapata ushindi hata mmoja katika mechi 13 walizocheza kwenye fainali za mashindano haya. Wamefungwa mechi nane na kutoka sare tano. Rekodi hiyo inaonesha wazi kwamba hatua inayofuata ya maendeleo ya Taifa Stars lazima ijikite kwenye kuongeza ubora wa mwisho mbele ya lango.

Ubora wa Morocco waongea kupitia Hakim na Díaz
Tofauti kati ya Tanzania na Morocco ilijitokeza wazi katika dakika ya 64 ya mchezo, pale Brahim Díaz alipofunga bao pekee la ushindi. Ilikuwa ni dakika chache tu baada ya Tanzania kupoteza nafasi yao nyingine muhimu, jambo linaloonesha jinsi soka la ushindani wa juu linavyoweza kuwa na ukatili wake.

Achraf Hakimi, kwa utulivu na ubora mkubwa, alitoa pasi iliyomkuta Díaz katika nafasi sahihi, na mshambuliaji huyo hakufanya makosa. Shuti lake kali lilipita upande wa kushoto wa mlinda mlango Hussein Masalanga. Kiwango cha juu cha umaliziaji kimeitofautisha Morocco na wapinzani wao katika mashindano haya.

Bao hilo lilikuwa la nne kwa Díaz katika AFCON 2025, akidumisha rekodi ya kufunga katika kila mechi aliyocheza katika fainali za mwaka huu. Hili linaonesha si tu ubora wake binafsi, bali pia mfumo wa Morocco unaowawezesha wachezaji wao muhimu kuamua mechi wakati inahitajika zaidi.

Baada ya bao hilo, Morocco hawakulazimika kushambulia kwa nguvu. Walitumia uzoefu wao, wakadhibiti mchezo kwa akili, wakipunguza kasi ya Tanzania hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa. Morocco sasa inatinga robo fainali na inakwenda kucheza na Cameroon.

Mwisho wa Safari, mwanzo wa somo kubwa kwa Tanzania
Ingawa Tanzania imetolewa katika raundi ya 16 bora, safari yao katika AFCON 2025 haiwezi kuitwa ya kushindwa. Kufuzu hatua hii kwa mara ya kwanza tayari ni mafanikio makubwa katika historia ya soka la taifa.

Zaidi ya hilo, ushindani waliouonesha Tanzania dhidi ya Morocco umeonesha kuwa pengo la ubora linaweza kupunguzwa kwa maandalizi sahihi. Walionesha ushindani pia dhidi ya Nigeria, Tunisia na uganda katika hatua ya makundi.

Hata hivyo, mechi hii imeweka wazi maeneo muhimu yanayohitaji maboresho makubwa. Ufanisi wa washambuliaji, uimara wa kiakili katika dakika muhimu, na uwepo wa wachezaji wengi zaidi wenye uzoefu wa kiwango cha juu ni mambo ambayo Tanzania italazimika kuyafanyia kazi kwa umakini mkubwa.

Kwa mashabiki wa Taifa Stars, maumivu ya kipigo hiki ni makubwa kwa sababu waliona uwezekano wa historia kubadilika. Lakini kwa mtazamo mpana, huu ni mwanzo wa imani mpya. Tanzania haikuondoka Rabat kama timu kibonde, bali kama timu iliyoshindana.

"Hatuwadai Stars, wamefanya zaidi ya kile tulichotarajia, maandalizi mazuri kwa ajili ya 2027," anasema Selemani Magima, shabiki wa Stars.

Ndoto ya Tanzania imeishia Morocco, lakini somo limepatikana. Na katika soka, mataifa yanayokua huanza kwa kujifunza namna ya kushindwa kwa heshima kabla ya kujifunza namna ya kushinda.

Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages