NEWS

Wednesday, 14 January 2026

Ofisi ya RMO Mara yaendesha semina ya Sikoseli Tarime



Sehemu ya watumishi wa afya wakifuatilia mada kwenye semina kuhusu ugonjwa wa Sikoseli iliyoendeshwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara mjini Tarime jana.

Na Godfrey Marwa
Tarime
-----------

Ofisi ya Mganga Mkuu Mkoa (RMO) wa Mara kwa kushirikiana na Halmashauri za Mji na Wilaya ya Tarime imeendesha semina ya ugonjwa wa Sikoseli kwa viongozi na wafanyakazi wa taasisi mbalimbali.

Semina hiyo ilifanyika mjini Tarime jana Januari 13, 2026, kwa ufadhili wa Shirika lisilo la Serikali la Tanzania Sickle-cell Disease Alliance (TSDA), ambapo ililenga kuongeza uelewa katika jamii kuhusu ugonjwa huo ili kuutokomeza nchini kufikia mwaka 2030.


Sehemu ya washiriki wa semina hiyo

Walioshiriki semina hiyo ni watoa huduma za afya ngazi ya jamii, walimu, viongozi wa dini, watendaji wa mitaa, wenyeviti wa mitaa na vijiji, wazazi na mashujaa wa Sikoseli (wanaoishi na ugonjwa huo) kutoka Halmashauri hizo mbili.

Mratibu wa magonjwa yasiyoambukizwa, Esther Muya kutoka Ofisi ya RMO alisema lengo mahsusi ni kuijengea jamii uwezo wa kuelewa ugonjwa wa Sikoseli ili tatizo lisiongezeke katika mkoa wa Mara wenye wagonjwa zaidi ya 6,000, huku wilaya ya Rorya ikiongoza ikifuatiwa na Tarime na Serengeti.

"Natoa wito kwa wananchi waweze kuja kwenye vituo vya afya wapime wajue hali zao, serikali imeshawekeza - imejitahidi kuleta vifaa kwenye vituo vya afya na hospitali zote zikiwemo za rufaa,” alisema.


Mratibu Esther Muya akizungumza na waandishi wa habari

Naye Shujaa wa Sikoseli, Neema Mohamed ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Bone and Blood Foundation inayotoa elimu ya Sikoseli na kuhamasisha watu kuchangia damu alisema ugonjwa ni wa kirithi.

“Mtoto anarithi vinasaba kutoka kwa wazazi wake wawili, kinasaba kimoja kinatoka kwa mama na kingine kwa baba, siyo kwa mzazi mmoja pekee.

"Mtoto mwenye Sikoseli anaweza kusoma akafikia elimu ya juu, mimi nina 'degree' kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam japo nina changamoto ya Sikoseli, niligundulika nikiwa na umri wa mika 10, mama hakuniacha nilihudhuria kliniki mpaka huku nilikofika.

"Kuna watu wana dhana potofu kuwa mtoto wa Sikoseli anapofikisha miaka 18 anafariki dunia, siyo kweli, mimi mpaka sasa nina miaka 35,” alisema Neema.


Shujaa wa Sikoseli, Neema Mohamed.

Wataalamu wa afya wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo kwa kuwa yamewaongezea uelewa juu ya ugonjwa wa Sikoseli na wameahidi kutoa huduma inayostahili kwa mashujaa wa Sikoseli ili kila mmoja aweze kuishi kwa furaha na kutimiza ndoto zake.


Wataalamu wa afya wakiwa katika picha ya p[amoja na mashujaa wa Sikoseli wakiwemo watoto na wazazi wao

Sikoseli ni ugonjwa wa kurithi unaoathiri chembechembe nyekundu za damu kwa hubadilika kuwa na umbo la mundu badala ya duara.

Mabadiliko haya husababisha damu kusafiri kwa shida kwenye mishipa na kupunguza usambazaji wa oksijeni mwilini.

Hali hii humfanya mgonjwa kupata maumivu makali ya mara kwa mara, uchovu, upungufu wa damu na kuugua mara kwa mara.

Ugonjwa wa sikoseli unaweza kudhibitiwa kwa uangalizi wa kitabibu, matumizi sahihi ya dawa na kuzingatia mtindo bora wa maisha.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages