NEWS

Monday, 5 January 2026

Mgodi wa Barrick North Mara waongoza kwa kuajiri wazalendo



Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma jana.

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
-------------

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo wilayani Tarime, mkoani Mara, ndiyo mgodi pekee nchini Tanzania ambao nafasi zote za juu za uongozi zinashikiliwa na wazalendo kwa asilimia 100, kwa mujibu wa taarifa ya serikali.

Kimsingi, na kutokana na mahitaji ya kupata uzoefu wa kukua kwa teknolojia duniani, kumekuwa na utaratibu wa kisheria wa urithishwaji wa Watanzania kushika nafasi za wataalamu wa kigeni, ikiwa ni jitihada za makusudi za kukuza ajira kwa wananchi wazawa.

Mgodi wa North Mara ambao unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals, umekuwa wa kupigiwa mfano kwa kuajiri Watanzania wengi katika ngazi mbalimbali.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, aliwambia waandishi wa habari jijini Dodoma jana kuwa miradi ya madini imeshuhudia ongezeko la idadi ya ajira kwa Watanzania kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi 18,853 kufikia Desemba 2024.
Waziri Mavunde alisema serikali inaendelea kufungua wigo wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini na kutenga eneo maalum la uwekezaji mahali ulipokuwa Mgodi wa Buzwagi wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, lenye ukubwa wa ekari 1,331.

Eneo hilo sasa litajengwa viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za migodini.

Mpaka sasa, Waziri Mavunde alisema viwanda sita vimekwishajengwa huku wamiliki 15 wakionesha nia ya kujenga viwanda vingine zaidi.

Waziri Mavunde aliipa changamoto sekta binafsi kuchangamkia fursa ya usambazaji wa huduma migodini ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Wakati huo huo, serikali kupitia Wizara ya Madini imetangaza rasmi orodha ya huduma na bidhaa za migodini zinazopaswa kutolewa kupitia kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100, kwa mujibu wa Waziri Mavunde.

Hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wazawa wanashiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages