
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo.
Musoma
--------------
Baada ya mafanikio makubwa ya usambazaji umeme kwenye vijiji vyote 68 vya jimbo la Musoma Vijijini, sasa msukumo mkubwa utakuwa kufikisha nishati hiyo kwenye vitongoji vyote 374.
Tayari kazi hiyo ya kupeleka umeme vitongojini inayotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imeshafikia asilimia 86.6, kwa mujibu wa Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge huyo, imeeleza kuwa kwa miradi ya Bajeti ya Mwaka 2025/2026, kazi kubwa itakuwa kukamilisha usambazaji umeme kwa vitongoji 50 vilivyobaki.
Taarifa hiyo ilisema wakandarasi wa kufanya kazi hiyo wameshapatikana na usambazaji umeme kwenye vitongoji hivyo umeanza.
Kwa upande wa umemejua, taarifa hiyo ikikariri taarifa ya REA, ilisema tayari wamepatikana wakandarasi wa kusambaza umemejua kwenye visiwa vilivyopo katika jimbo hilo.
Wananchi na viongozi wa Musoma Vijijini wanaishukuru serikali kwa kuendelea kugharimia miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.
Pia, REA imepongezwa kwa kazi nzuri ya kusambaza umeme katika jimbo hilo lililopo mkoani Mara.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment