
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, akizungumza wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma jana.
Musoma
-------------
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amesema serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya chakula kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) inayotekelezwa nchi nzima katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Silinde aliyasema hayo Musoma jana, wakati wa uzinduzi wa vifaa vya kisasa vya kilimo cha umwagiliaji ili kuimarisha sekta hiyo, hususan kilimo cha umwagiliaji na matumizi sahihi ya teknolojia kwa vikundi vya wakulima.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wakulima wanapata zana na maarifa sahihi ya teknolojia na mbinu zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuwekeza fedha katika sekta ya kilimo mkoani Mara na kuongeza ustawi wa wananchi kwa kutumia rasilimali zilizopo, hususan Ziwa Victoria.
“Moja ya adhima ya serikali ni kuhakikisha sekta ya kilimo inakua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, ambapo miradi 20 tayari imeidhinishwa katika awamu ya kwanza kwa mikoa ya Dodoma, Manyara, Tabora, Geita, Lindi na Mara,” alisema Silinde.
Alisema mradi huo utagharimu takriban Dola za Kimarekani milioni 300, huku serikali ikiendelea kutekeleza vipaumbele vya kuongeza tija na uzalishaji kupitia utoaji wa pembejeo za ruzuku, mbegu bora, upimaji wa afya ya udongo, matumizi ya teknolojia za kisasa na ujenzi wa miradi mikubwa ya kilimo cha umwagiliaji.
Aliongeza kuwa kipaumbele kingine ni kuongeza ajira zenye staha kwa kushirikisha vijana na wanawake, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya nje, kuimarisha vyama vya ushirika na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika maendeleo ya sekta ya kilimo.

Naibu Waziri Silinde akizindua vifaa vya kisasa vya kilimo cha umwagiliaji katika Manispaa ya Musoma jana
Naibu Waziri Silinde alisema serikali pia imepanga kujenga skimu za umwagiliaji nchi nzima ili kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali, yakiwemo mboga na matunda.
Alifafanua kuwa skimu hizo zitatekelezwa katika mikoa 15, wilaya 45 na majimbo 65, ambapo wakulima zaidi ya 4,000 watanufaika.
Naye Mratibu wa TFSRP, Timotheo Semuguruka, alisema programu hiyo inalenga kusimamia upatikanaji wa huduma bora za ugani kwa kutoa elimu, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora na kuendeleza umwagiliaji mkubwa na mdogo kwa kuzingatia matumizi sahihi ya maji ya juu na ya chini ya ardhi, pamoja na kuhifadhi rutuba ya udongo na usalama wa chakula.
“Rais anasisitiza matumizi sahihi na endelevu ya rasilimali tulizonazo, kama mnavyoona tupo karibu na ziwa,” alisema Semuguruka.
Kwa upande wake Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Haji Mtete, alimshukuru Naibu Waziri Silinde kwa ziara hiyo na juhudi zake za kuimarisha sekta ya kilimo.
Mtete alisema hatua hiyo itawawezesha wakulima kuongeza uzalishaji, kipato, usalama wa chakula na kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa wakulima wa eneo hilo.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Aines Kamugisha, akitoa taarifa ya utekelezaji wa kilimo cha umwagiliaji katika halmashauri hiyo, alisema shughuli za ugani zimekuwa zikihusisha kutembelea na kutoa ushauri kwa wakulima juu ya kanuni bora za kilimo na kuwasajili kwenye mfumo wa kidijitali.
Kamugisha alisema wakulima 1,127 wamesajiliwa katika mfumo huo, hatua inayowawezesha kununua mbolea na mbegu za serikali pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu kwa njia ya mtandao.
Pia, alibainisha kuwa wakulima wamehamasishwa kutumia vyakula vyenye lishe bora vinavyorutubisha mwili kwa njia za kibaiolojia.
Alisema vikundi vinane kutoka Manispaa ya Musoma vimewezeshwa kwa kupatiwa vifaa vya kisasa vya kilimo cha umwagiliaji kwa ajili ya uzalishaji wa mbogamboga na matunda.
No comments:
Post a Comment