
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, DCP David Misime.
Jeshi la Polisi linachunguza matukio matatu ya vifo vilivyotokea kwa nyakati tofauti nchini, likiwemo la Dickson Tadeus Joseph, mkazi wa Rebu mjini Tarime, Mara.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini jana, ilieleza kuwa kijana huyo alifariki dunia Januari 1, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, akidaiwa kuuawa na askari polisi.
“Uchunguzi wa kina umeanza, na kulingana na ushahidi kutoka kwa watu walioshuhudia – ikibainika kuna askari aliyehusika hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Tukio la pili linalochunguzwa ni la raia wa Rwanda, Viollete Uwumuhoza, anayedaiwa kujinyonga Januari 7, 2026 akiwa mahabusu ya Polisi jijini Arusha alikokuwa akishikiliwa kwa tuhuma za kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria.
Pia, Jeshi la Polisi linamshikilia askari polisi mmoja katika Mkoa wa Kipolisi Rufiji kwa tuhuma za kumuua kwa risasi Shaban Said Luluba, mkazi wa Nyamwage wilayani Rufiji, wakati akifanya ukamataji Januari 8, 2026.
No comments:
Post a Comment