
Upandaji wa miti ya asili ukiendelea kando kando ya mto Tighite katika kijiji cha Matongo
Tarime
-------------
Miti zaidi ya 40,000 imepandwa kando kando ya mto Tighite kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime, mkoani Mara.
Hatua hiyo ni sehemu ya programu maalum inayotekelezwa na pande hizo mbili kuhifadhi mazingira na kurejesha ikolojia kama si uoto wa asili wa mto huo.
Mto Tighite ni moja ya vyanzo vikuu vya maji vya Mto Mara ambao unatiririsha maji yake katika ziwa la kimataifa - Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tigithe Chini (JWMTC), Mwita Seri, ameeleza kufurahishwa na ushirikiano anaopata kutoka Barrick North Mara katika kutekeleza mpango wa kuhifadhi mazingira ya mto huo.
“Barrick wanatupatia ushirikiano mkubwa sana. Meneja Mkuu na Meneja wa Mazingra pamoja na watalaamu wanatupatia ushirikiano mzuri sana. Hadi sasa tumeshapanda miti ya asili 42,700.
“Kwa kweli tumefurahi, na sasa hivi watu, yaani jamii inawaona Barrick kama mdau mzuri wa kuhifadhi mazingira kwa kushirikiana na jamii,” Seri aliwambia waandishi wa habari, wiki iliyopita.
Aliongeza kuwa mgodi huo umeendelea kushirikiana na jumuiya yake katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo tangu walipouzindua wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka jana [2025].
“Mwanzoni sikuamini, lakini nilipopeleka andiko la kuomba support ya kuhifadhi mazingira ya mto Tighite lilipokelewa na Barrick - kazi ikaanza bila kuchelewa,” alisema.

Sehemu ya miche ya miti ya asili iliyooteshwa kwenye kitalu cha Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini kwa ajili ya kupandwa kando kando ya mto Tighite.
Kwa mujibu wa Seri, uharibifu mkubwa wa uoto wa asili wa mto Tighite ndio uliisukuma jumuiya yake kubuni wazo la kuwa na mpango endelevu wa kuhifandi mazingira ya chanzo hicho cha maji.
“Lengo kubwa ni kulinda mto Tighite kwa kurudisha uoto wa asili, na hata miti tunayopanda ni ya asili na rafiki kwa mazingira,” alisema Mwenyekiti huyo wa JWMTC.
Alisema mgodi wa Barrick North Mara unagharimia ununuzi wa miche ya miti, uchimbaji mashimo na ulinzi wa miti iliyopandwa, miongoni mwa mambo mengine katika mradi huo.
Alibainisha kuwa Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini ambayo iko chini ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, inasimamia kata nne zenye vijiji 12 jirani na mgodi wa Barrick North Mara.
Alitaja vijiji hivyo na kata zake zikiwa kwenye mabano kuwa ni Matongo, Nyabichune, Nyangoto na Mjini Kati (Matongo), Nyamwaga na Komarera (Nyamwaga).
Vijiji vingine ni Nyakunguru, Nyarwana, Wegita na Keisaka (Kibasuka), Kewanja na Kerende (Kemambo).
Seri alisema maelfu ya wakazi wa vijiji hivyo wanategemea mto Tighite kupata maji ya matumizi ya nyumbani, kunywesha mifugo na shughuli za kilimo.
Hivyo, juhudi za pamoja za JWMTC na Barrick North Mara katika uhifadhi endelevu wa mazingira ya mto huo zitasaidia kuimarisha upatikanaji wa maji kwa ustawi wa maisha ya binadamu na viumbe hai wengine.
Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment