NEWS

Sunday, 8 February 2026

Mwenyekiti wa CCM Mara ashiriki mazishi ya diwani aliyefariki dunia kwa ajali Tarime



Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa (wa pili kushoto), akiwasili kushiriki mazishi ya Diwani Philipo Marwa Gikaro katika mtaa wa Kibumaye, nje kidogo ya mji wa Tarime, leo Februari 8, 2026. (Picha na Mara Online News)

Na Mwandishi wetu
Tarime
------------

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, leo Februari 08, 2026 ameshirki katika mazishi ya Diwani wa Kata ya Ketare iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime, Philipo Marwa Gikaro.

Mazishi hayo yanafanyika nyumbani kwa marehemu katika mtaa wa Kibumaye, nje kidogo ya mji wa Tarime, ambapo Mwenyekiti Chandi amewapa pole familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na mpendwa wao.

Naye Mwenyekiti Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho tawala, Fadhili Maganya, mbali na kuwapa pole wafiwa, ametumia nafasi hiyo pia kuitaka Halmashauri ya Mji wa Tarime kushughulikia ubovu wa barabara ya Tarime Mjini-Mogabiri.

"Natoa maelekezo, tumieni mapato ya halmashauri kuondoa kero ya barabara hiyo. Nimetoa maelekezo kwa DC (Mkuu wa Wilaya) na Mkurugenzi wako myachukue haya na kuyasimamia,” ameagiza Maganya.


Maganya akizungumza katika msiba huo


Mwenyekiti Chandi akisaini kitabu cha rambirambi kwenye msiba huo

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Elias Ghati na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Gimbana Natavyo, pia wanashiriki katika msiba huo ambao umehudhuriwa na mamia ya wananchi.

Vilevile, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daud Ngicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayumb Mwita Makuruma na Mwenyeketi wa Hamashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Matera Chacha, nao pia wamehudhuria mazishi hayo.


Makuruma akisaini kitabu cha salamu za rambirambi msibani hapo


Matera akisaini kitabu cha salamu za rambirambi kwenye msiba huo

Wengine walioshiriki mazishi hayo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kemanyanki Contractors, Nicolaus Mahando Mgaya “Chichake” na Mkurugenzi wa Soya One Limited, Chacha Soya.


Chichake akisaini kitabu cha salamu za rambirambi msibani hapo


Chacha Soya akisaini kitabu cha salamu za rambirambi msibani hapo

Philipo ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Ketare kwa tiketi ya CCM, alifariki dunia baada ya kupata ajali ya kugongwa na gari Jumanne iliyopita katika eneo la Kibumaye wakati akielekea nyumbani kwake Mogabiri, muda mfupi baada ya kuhudhuria kikao cha Barabza la Madiwani kilichopitisha rasmu ya bajeti ya Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa mwaka 2026/2027.


Philipo akishiriki kikao cha Baraza la Madiwani saa chache kabla ya kupata ajali iliyomsababishia mauti

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages