
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (katikati aliyevaa kofia), akiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (aliyevaa suti ya bluu), juzi alipokwenda kukagua miradi ya kimkakati ya sekta ya uchukuzi inayotekelezwa katika mkoa huo. Kulia mbele ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.
Mara
-------------
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amezungumzia miradi mikubwa ya kimkakati ya sekta ya uchukuzi iliyoanza kutekelezwa mkoani Mara, itakavyoifungua mikoa ya Kanda ya Ziwa kiuchumi na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.
Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani hapa juzi, Waziri Mbarawa alitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma na ujenzi wa Uwanja wa Ndege Serengeti.
Miradi mingine ni upanuzi wa Bandari ya Musoma na ujenzi wa reli ya SGR ambayo ikikamilika itaiunganisha Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.
“Miradi hii ina manufaa makubwa sana katika uchumi wa mkoa wa Mara, mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla, kwa kuwa itaziunganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda katika usafiri wa uhakika, kuchochea uchumi na kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania,” alisema Waziri Mbarawa.

Waziri Mbarawa alisema mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma upo katika hatua nzuri kwani njia ya kurukia ndege imekamilika, jambo ambalo litasaidia safari za ndege kuanza wakati baadhi ya maboresho yakiendelea katika uwanja huo, ikiwemo ujenzi wa jengo la abiria na kufunga taa ili kuuwezesha kufanyakazi saa 24.
Aidha, aliahidi kuharakisha kulipa madai ya mkandarasi anayejenga uwanja huo ili akamilishe kazi haraka, hususan kujenga mtaro karibu na njia ya kutua ndege ili uweze kuanza kutumika kwa ndege kubwa za abiria.
Kuhusu Bandari ya Musoma, Prof. Mbarawa alisema serikali inakusudia kujenga gati mpya litakaloiwezesha meli ya MV Mwanza na nyingine za abiria na mizigo kufanya safari na kusimama katika bandari hiyo.
Alisema mpango wa serikali ni kuiunganisha na Bandari ya Musoma na Bandari ya Tanga, na kwa usafiri wa reli ya SGR kutoka Tanga- Arusha hadi Musoma ili kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Tanga kwenda Uganda kupitia Bandari ya Musoma, hivyo kufungua uchumi wa mkoa wa Mara.

Kuhusu Uwanja wa Ndege Serengeti, Waziri Mbarawa alisema ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya upembuzi yakinifu kukamilika na kwamba utakuwa wa kibiashara kwani utawavutia watalii wengi kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, aliiomba Wizara ya Uchukuzi kuanza upanuzi wa Bandari ya Musoma ambayo itaunganisha usafiri kwenda miji ya Kisumu (Kenya) na Entebe (Uganda), hivyo kuufungua mkoa huo kiuchumi.
RC Mtambi alisema upanuzi wa Bandari ya Musoma upo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030, ambapo mradi huo na ujenzi wa reli ya SGR kutoka Tanga- Arusha hadi Musoma utasaidia katika kuchechemua biashara za ndani na nje ya nchi.
“Bandari hii itatusaidia sana wananchi wa mkoa wa Mara kuwa na usafiri wa majini wenye uhakika na utapunguza gharama za bidhaa na kuchochea biashara mbalimbali katika nchi hizi,” alisema.
Pia, RC Mtambi aliiomba Wizara ya Uchukuzi kuanzisha safari za ndege kubwa za abiria katika Uwanja wa Ndege Musoma, hususan za kwenda Mwanza, Dar es Salaam, Zanzibar na Dodoma, ili kurahisisha usafiri wa watu na mizingo, wakiwemo watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.
“Kwa sasa watalii wanaoingia Hifadhi ya Taifa Seregeti wanalazimika kupita nchi jirani ya Kenya, mkoa wa Arusha au Mwanza ili kuweza kuingia hifadhini kwa urahisi, jambo ambalo linawakwamisha baadhi ya watalii kuingia katika hifadhi hiyo kutokana na gharama za usafiri kuwa kubwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mshauri Mwelekezi wa mradi wa upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma, Mhandisi Ezra Magogo, alisema kwa sasa uwanja huo una barabara ya kurukia ndege yenye urefu wa mita 1,705 na upana wa mita 45, na kwamba mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo umenika asilimia 60 ya utekelezaji wake.
“Mkandarasi kwa sasa anadai malipo ya shilingi bilioni 1.9 yaliyopo wizarani na shilingi bilioni 2.5 zimepokelewa na yanaendelea kuhakikiwa na wataalamu kabla ya kupelekwa wizarani kwa ajili ya malipo,” alisema Mhandisi Magogo.
Alibainisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 36.3 ukihusisha njia ya kurukia ndege, jengo la zimamoto, majengo ya ofisi, nyumba za watumishi na barabara za kuzunguka uwanja huo.
Hata hivyo Mhandisi Magogo alisema changamoto kubwa za uwanja huo kwa sasa ni mtaro unaohitajika kujengwa kwa gharama ya shilingi milioni 280 ili kutoa usalama zaidi kwa ndege wakati wa kutua, ili ndege za abiria ziweze kuanza kuutumia.
Katika ziara hiyo, Waziri Mbarawa alitembelea pia ofisi za CCM Mkoa wa Mara na kupokelewa na Kamati ya Siasa ya Mkoa ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Patrick Chandi Marwa.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment