NEWS

Sunday, 22 February 2026

CMG Hotels - Tarime yaibuka mshindi Tuzo ya Hoteli Bora Kanda ya Ziwa



Meneja Mkuu wa CMG Hotels – Tarime, Vicent Karanja (aliyevaa tai nyekundu) na Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Hoteli hiyo, Anicet Marwa (kulia), awakionesha Tuzo na Cheti kwa ushindi huo.

Na Mwandishi Wetu
Mwanza
---------------

CMG Hotels - Tarime iliyopo mkoani Mara imeibuka mshindi wa Tuzo ya Hoteli Bora Kanda ya Ziwa (Lake Zone Best Hotel Award) katika mashindano maalum yaliyoandaliwa na Wadau Shupavu Awards kwa ufadhili wa Holy Smile.

CMG Hotels - Tarime imetwaa tuzo hiyo ikizishinda hoteli nyingine kadhaa kutoka mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu zilizoshiriki mashindano hayo.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa Februari 16, 2026 katika hafla maalum iliyofanyika kwenye Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza, ambapo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa CMG Hotels - Tarime, Anicet Marwa, alisema ushindi huo ni matunda ya uwekezaji katika huduma bora kwa wateja.

“Tunajivunia ushindi huu mkubwa, umetokana na huduma bora, nidhamu ya kazi na kujali mahitaji ya wateja wetu wakati wote,” alisema Marwa.

Alibainisha kuwa hiyo ni tuzo ya pili kwa CMG Hotels - Tarime ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu ifunguliwe rasmi, kwani Septemba 28, 2025, ilitunukiwa Tuzo ya Heshima (Honorary Award) Mkoa wa Mara.

Alisema hoteli hiyo imeendelea kujiimarisha kwa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wageni wa ndani na nje ya Tanzania.

Alitaja huduma hizo kuwa ni malazi, chakuna, vinywaji, kumbi za mikutano, ukumbi wa mazoezi ya mwili (gym), sauna, kuogelea kwenye mabwawa ya kisasa na maegesho ya magari, miongoni mwa nyingine.


Sehemu ya muonekano wa mbele wa CMG Hotels - Tarime

Marwa alitoa wito kwa wateja kuendelea kujitokeza kwa wingi kufurahia huduma za hoteli hiyo katika mazingira ya kuvutia na usalama mkubwa.

Alisema ushindi wa tuzo hizo ni chachu ya kuongeza ubunifu na kuimarisha zaidi ubora wa huduma za CMG Hotels - Tarime.

“Tunawakaribisha wateja wetu wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuja kufurahia huduma zetu zenye viwango vya juu. Tupo kwa ajili yao,” alisisitiza Marwa.

Ushindi wa tuzo hiyo unaongeza hadhi ya CMG Hotels - Tarime kama hoteli inayoongoza kwa huduma za viwango vya juu katika Kanda ya Ziwa, hivyo kuifanya kuwa chaguo sahihi kwa wasafiri wa kibiashara na mapumziko.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages