NEWS

Sunday, 22 February 2026

Nyansaho Foundation, Mbunge Mary wawapa tabasamu wanafunzi 361 wa kidato cha kwanza Serengeti



Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Joseph (kulia) na Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema (aliyevaa kofia), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi waliopata msaada wa vifaa kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza wilayani Serengeti.

Na Mwandishi Wetu
Serengeti
----------------

Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundation - NF) kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Serengeti imegawa msaada wa vifaa mbalimbali vya shule vyenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 60 kwa wanafunzi 361 wa kidato cha kwanza.

Wanafunzi hao ni ambao wanatoka mazingira magumu katika jimbo hilo, walioshindwa kuripoti katika shule zao mwaka huu wa 2026.


Baadhi ya wanafunzi waliojitokeza kupokea msaada wa vifaa ili waweze kuripoti shule kuanza na masomo ya kidato cha kwanza.

Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ilifanyika jana Jumapili katika Stendi ya zamani ya Serengeti na kuhudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa chama, serikali na wananchi wa kawaida.

Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Joseph, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema ofisi yake kwa kushirikiana na Nyansaho Foundation itahakikisha watoto wanaotoka mazingira magumu hawakosi haki ya kupata elimu kwa kukosa mahitaji ya shule.


Mbunge Mary (aliyeshika begi) akigawa vifaa vya shule kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza.

"Ofisi yangu kama Mbunge tutaendelea kutoa ushirikiano, na kupitia Nyansaho Foundation tutahakikisha tunaendelea kufikia watoto wengi zaidi.

"Maendeleo yanaletwa na elimu. Wazazi, wananchi wenzangu, wapenda maendeleo mnisaidie… watoto wanaotakiwa kuripoti wapelekwe shuleni.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweza kufutilia mbali ada ili kuhakikisha watoto wanaotoka mazingira magumu na kaya masikini tunapata haki ya kwenda shule na kupata elimu,” alisema Mbunge Mary.

Kwa upande wake Mratibu wa Nyansaho Foundation Kanda ya Ziwa, Modester Mwema, alimshukuru Mbunge Mary kwa kuonesha ushirikiano na kutambua watoto wanaohitaji kupata elimu ili kutimiza ndoto zao.

Modester alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wazazi na walezi kuhakikisha kuwa msaada wa vifaa hivyo unakuwa chachu ya watoto kwenda kuripoti shule.

"Kama Nyansaho Foundation, tunamshukuru Mbunge, lakini pia Mkurugenzi wa Taasisi, Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho, kuendelea kutuhamasisha kama wadau wa maendeleo na kujiona kama sehemu ya wananchi wanaotoka mazingira magumu, na kwa kunyoosha mkono kwa ajili ya watoto na kuleta tabasamu, lengo kubwa waende shule.

"Tunawasihi wazazi muendelee kuhamasisha watoto, vifaa vilivyotolewa iwe ni chachu ya kuendelea na masomo zaidi, na kama taasisi tutaendelea kuwafuatilia,” alisema Mratibu huyo wa Nyansaho Foundation.

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu (2026) katika wilaya ya Serengeti ni 5,250 lakini walioripoti shule mpaka sasa ni 3,975 sawa na asilimia 76. Waliobaki hawajaripoti kutokana na sambabu mbalimbali, ikiwemo kukosa mahitaji muhimu ya shule.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages