NEWS

Saturday, 7 February 2026

Wananchi walia kero ya ubovu wa barabara ya Tarime Mjini–Mogabiri kufumbiwa macho




Na Mwandishi Wetu,
Tarime
-------------

Barabara ya Tarime Mjini–Mogabiri (kilomita sita) imeendelea kuwa kero kubwa kwa watumiaji wake, baada ya kugeuka kuwa hatarishi kutokana na kujaa mashimo yaliyochimbika kwenye lami.

Wananchi wakiwemo madereva wanaotumia barabara hiyo kila siku wanasema tatizo hilo limekuwepo kwa miaka kadhaa sasa bila hatua madhubuti kuchukuliwa, licha ya barabara hiyo kuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Mashimo yaliyotapakaa kwenye kipande hicho cha barabara yamesababisha usumbufu mkubwa kwa vyombo vya usafiri, yakiwemo magari, malori ya mizigo, pikipiki, baiskeli na hata watembea kwa miguu.

Wakati wa mvua, mashimo hayo hujaa maji na kuwa mitego isiyoonekana, hali inayoongeza hatari ya ajali na uharibifu wa vyombo vya usafiri.

“Tumeshuhudia ajali ndogondogo na kubwa zikitokea hapa, hasa usiku. Dereva anaepuka shimo moja, anaingia jingine. Ni hatari sana,” mmoja wa waendesha ‘bodaboda’ wanaotumia barabara hiyo ameiambia Mara Online News, leo Jumamosi.

Barabara hiyo ni njia kuu ya kusafirisha mazao ya kilimo na mifugo kutoka maeneo ya vijijini kwenda masoko yaliyopo mjini na nje ya wilaya ya Tarime, lakini pia hutumiwa na watalii kutoka nchi jirani ya Kenya wanaokwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti, moja ya vivutio vikubwa vya utalii barani Afrika.

Aidha, ni sehemu ya barabara inayoelekea maeneo ya Nyamongo, ambako shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinafanyika na kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa wananchi na pato la taifa.

Hali ya barabara hiyo si tu kwamba inahatarisha maisha ya watumiaji, bali pia inadumaza maendeleo ya kijamii na kiuchumi - kwa kuongeza gharama za usafirishaji, kuchelewesha huduma na kuharibu taswira ya mji wa Tarime kwa wawekezaji na watalii.

Wananchi sasa wanazitaka mamlaka husika, ikiwemo TANROADS na TARURA kuchukua hatua za haraka kurekebisha barabara hiyo kabla haijasababisha maafa makubwa zaidi.

“Ni aibu barabara muhimu kama hii kuachwa katika hali mbaya kwa muda mrefu. Tunahitaji suluhisho la kudumu, si kuziba mashimo kwa kutumia udongo pindi zinapokaribia ziara za viongozi wa juu serikalini,” amesema mkazi wa Mogabiri, aliyejitambulisha kwa jina la Wambura.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kuzipata mamlaka zinazohusika ili kujua kama zina mpango wowote wa kutimiza wajibu wao wa kurejesha hadhi ya barabara ya Tarime Mjini–Mogabiri iwe salama na kurahisisha usafiri kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages