NEWS

Friday, 6 February 2026

Ndege za ATCL kuanza kutua Musoma




Na Mwandishi Wetu
Dodoma
-----------------

Ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zitaanza kufanya safari za majaribio ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Musoma baada ya kufanyiwa uboreshaji na upanuzu wa viwango vya juu, serikali imesema.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, majaribio hayo yanatarajiwa kuanza Machi, au Aprili 2026.

Naibu Waziri Kihenzile alisema tayari ujenzi wa ‘runway’ umekamilka katika uwanja huo uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma - makao makuu ya mkoa wa Mara.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa Mkoa wa Mara iliaza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mara [Musoma], na pale serikali inajenga runway - kwa maana ya njia ya kuruka na kutua ndege, tayari runway imekwisha kamilika,” Kihenzile alisema Bungeni jijiji Dodoma Februari 3, 2026.

Alisema ndege za ATCL zitafanya majaribio katika viwanja vya ndege vingine vya Shinyanga na Sumbawanga.

“Hii ni kuthibisha dhamira ya Dkt. Samia [Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan] kuwa ameamua kuitendea haki setka ya anga,” alisema Kihenzile.

Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu swahili la Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege, aliyetaka kujua ni lini Uwanja wa Ndege Musoma - ambao alisema ni kielelezo cha mkoa wa Mara utakamilika.


Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege, akizungumza Bungeni jijini Dodoma.

Naibu Waziri Kihenzile alisema ujenzi wa majengo mengine katika uwanja huo unaendelea.

Uboreshaji na upanuzu wa Uwanja wa Ndege Musoma unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mkoa wa Mara.

Uwanja huo utawezesha ndege kubwa kutua katika mji huo na hivyo kurahisisha safari kwa watalii wanaotembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa huo, ikiwemo hifadhi bora Afrika - Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Taarifa zinaonesha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia umewekeza takariban shilingi bilioni 35 kutekeleza mradi huo.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages