NEWS

Saturday, 7 February 2026

Jinsi ya kuboresha uwekezaji Kanda ya Ziwa



Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akifungua Kongamano la Uwekezaji Kanda ya Ziwa.

Na Mwandishi Wetu,
Mwanza
----------------

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetakiwa kuwa chombo imara cha kuboresha mazingira ya biashara kwa kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje.

TISEZA itaweza kutimiza jukumu hilo iwapo itashirikiana kwa karibu na sekretarieti za mikoa na sekta binafsi kuwawezesha wananchi kushiriki katika uwekezaji.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji Kanda ya Ziwa jijini Mwanza, Jumatano Februari 4, 2026.

Waziri Kapinga alisema lengo la serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi tatu za Afrika katika kuvutia uwekezaji na kuwa nchi yenye mazingira bora ya kufanya biashara ifikapo 2050.

Kongamano la Uwekezaji la Mwanza liliandaliwa na TISEZA kujadili maeneo muhimu ya vitega uchumi kwa kanda hiyo.

Kanda hiyo inajumuisha mikoa sita; ambayo ni Geita, Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu.

Mikoa hiyo inahesabika ni kitovu cha uwekezaji kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini, hasa dhahabu na almasi.

Pia, mikoa hiyo inasifika kwa kilimo cha mazao ya biashara kama vile pamba na kahawa, pamoja mazao ya chakula.

Kutokana na uwepo wa Ziwa Victoria, shughuli za uvuvi ni kivutio kikubwa kinachochangia pato la taifa.

Kwa miongo mingi, mikoa ya Kanda ya Ziwa inategemea pia ufugaji na shughuli za utalii kwenye hifadhi za taifa, ikiwemo hifadhi kongwe na bora Afrika – Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages