NEWS

Saturday, 28 February 2026

RC Mtambi azungumza na waliogomea uthamini, fidia Mgodi wa North Mara, awapa siku saba kuweka mambo sawa



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (wa pili kushoto mbele), akiwasili Nyamongo katika moja ya maeneo ambapo wananchi wamegomea uthamini na fidia. Wa kwanza kushopto ni Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko, miongoni mwa viongozi wengine.

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Nyamongo
--------------------

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka wananchi waliogomea uthamini na malipo ya fidia ili kupisha Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuhakikisha wanatengua msimamo huo ndani siku saba.

RC Mtambi alitoa agizo hilo Februari 27, 2026, alipofika Nyamongo wilayani Tarime na kuzungumza na baadhi ya wananchi hao.


RC Mtambi (katikati) akiwa katika kitongoji cha Nyabikondo, Nyamongo kwenye makazi ya mmoja wa wananchi waliogomea uthamini.

“DC (Mkuu wa Wilaya) na watu wa ardhi nawapa siku saba kuanzia Jumatatu, mje kwa hawa wananchi, mkae nao muwaelimishe wakubali kufanyiwa uthamini na kupokea fidia kwa mujibu wa sheria,” alisema RC Mtambi.

Alionya kuwa kugomea uthamini na fidia kunakiuka sheria za nchi na kunachelewesha shughuli za mgodi huo pamoja na miradi ya maendeleo inayotegemea uwekezaji huo.
“Wanakwamisha mwekezaji na maendeleo ya wananchi, hii haikubaliki, mali iliyopo chini ya ardhi ni mali ya serikali, tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria na kwa manufaa ya wananchi,” RC Mtambi alisisitiza.

Awali, Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko, alimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba kati ya wananchi 75 wanaotajwa, baadhi wamegoma kufanyiwa uthamini na wengine wamekataa kupokea malipo ya fidia za mali zao licha ya kufanyiwa tathmini na kusaini mikataba ya makubaliano.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.


Lori likiwa kazini katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara

Mgodi huo ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa uchimbaji wa madini nchini, ambao unachangia utekelezaji wa miradi ya kijamii, mapato ya taifa na ajira kwa Watanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages