NEWS

Wednesday, 25 February 2026

Mambo yaiva ujenzi Uwanja wa Ndege Serengeti



Sehemu ya eneo lilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege Serengeti

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeomba mkopo kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ambapo sehemu ya mkopo huo itatumika kugharimia ujenzi wa Uwanja wa Ndege Serengeti, mkoani Mara.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa TAA, tenda ya ujenzi wa uwanja huo inapitia taratibu zote kama zinavyoelezwa kwenye kifungu 410 cha Sheria ya Ugavi na Kanuni nyingine.

Wakandarasi watakaohitaji kushiriki katika tenda hiyo wanatakiwa kutuma maombi yao kupitia mfumo wa kidijitali wa ugavi (NeST), tangazo la TAA limeeleza.

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Serengeti, ambao umesuasua kwa miongo zaidi ya miwili, umo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2025-2030.

Nia ya ujenzi wa uwanja huo ni kuugeuza mji wa Serengeti kuwa kitovu cha utalii kwani unapakana na hifadhi bora Afrika - Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Ujenzi wa uwanja huo utawawezesha watalii kutoka nje kutua moja kwa moja katika mji wa Serengeti na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Mara.

Pia, ujenzi wa mradi huo wa kimkakati utapunguza idadi ya ndege zinazotua ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Uimarishaji wa viwanja vya ndege ni mkakati maalum wa Serikali ya Tanzania wa kuvutia wawekezaji katika kila sekta ya kiuchumi.

Sasa hivi, viwanja kadhaa vya ndege nchini vimo katika mipango ya serikali ya kuviboresha ili vikidhi mahitaji ya sekta ya usafiri wa anga.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages