
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba (wa pili kulia), akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka (wa pili kushoto), mfano wa hundi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwezesha vijana na wanawake. Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi (kushoto) na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar (kulia).
Dodoma
----------------
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekabidhi hundi ya shilingi bilioni 200 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, ikiwa ni mtaji wa kuwawezesha vijana na wanawake nchini.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu - Mlimwa jijini Dodoma, jana Alhamisi, Februari 5, 2026.
Fedha hizo ni ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya mtaji wa kuwainua vijana na wanawake kiuchumi.
"Utoaji wa hundi ya shilingi bilioni 200 unaonesha kwa vitendo kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza ahadi zake kwa vitendo. “Ni msingi wa kuimarisha ushiriki wa vijana na wanawake katika uchumi wa taifa," alisema Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu.
Alisema uwezeshaji wa vijana na wanawake lazima uwe chombo cha mageuzi ya kiuchumi na kuonya kwamba serikali "haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka dhamira ya uwezeshaji huu."
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, alisema changamoto ya upatikanaji wa mitaji, ikiwemo mikopo, vifaa, mashine na mitambo bado ni kikwazo kwa ukuaji uchumi.
Kutokana na chagamoto hiyo, Rais Dkt. Samia ameongeza shilingi bilioni 200, kwa ajili ya kuwezesha vijana na wanawake, alisema Waziri Lukuvi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar na mwaziri wegine kadhaa, miongoni wa viongozi wengine.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment