
Na Godfrey Marwa
Tarime
-----------------





Tarime
-----------------
Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA) Wilayani Tarime limeonesha tendo la mapendo kwa kuandaa futari ya pamoja na Waislamu wa wilaya hiyo.
Futari hiyo ilifanyika Februari 27, 2026 katika Chuo cha Ualimu Tarime (TTC) na kuhudhuriwa pia na viongozi mbalimbali, ikilenga kuendeleza na kudumisha uhusiano kati yao kwa maendeleo ya Tarime na Taifa.

Mwenyekiti wa Jimbo Dogo la North Mara Field (NMF), Mchungaji Dkt. Benjamin Ngaramabiha, alisema wanalenga kuungana kudumisha uhusiano na amani, miongoni mwa waamini wa madhehebu hayo.
"Kusudi letu kubwa tumekuja kuungana na ndugu zetu Waislamu ambao wapo katika utekelezaji wa nguzo muhimu sana ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani," alisema.

"Tumekuja kudumisha mahusiano tufahamiane tutakiane heri na baraka, na jambo kubwa kama Watanzania tunayo tunu adhimu nayo ni amani tuilinde mana ukiipoteza ni gharama kuilipa.
"Tudumishe amani, umoja, upendo, tuishi kama ndugu na tukifanya hivyo tutaona matokeo chanya katika wilayani yetu ya Tarime," alisema Mchungaji Ngaramabiha.

Naye Sheikh wa Wilaya ya Tarime, Masoud Said Wambura, alisema wao kama Waislamu wamefurahi kujumuika na Wasabato katika iftari hiyo ya pamoja.
"Nitoe shukrani kwa niaba ya Waislamu wa Tarime kuwa sote tumefurahishwa na tukio hili, kwa kuona kuwa kuna haja ya kushirikiana kujumuika kupata futari pamoja, kuadhimisha futari ndiyo maelekezo ya Mwenyezi Mungu na mitume wake.
"Kama Watanzania tunapaswa kuwa wamoja, kushirikiana kuilinda na kuhifadhi amani ya nchi yetu, kwani bila amani hiyo tusingeweza kukutana hapa," alisema Sheikh Wambura.


No comments:
Post a Comment