NEWS

Monday, 3 August 2026

Harambee ya Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga yavuna shilingi milioni 259



Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila, akiwapongeza Mama Leah (kulia) na Anita Gimero Waitara (katikati) kwa michango waliyotoa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa jipya la Parokia ya Nyamwaga jana Jumapili. Kushoto ni Paroko wa Parokia hiyo, Padre Julius Manyonyi.

Na Godfrey Marwa
Tarime
------------

Shilingi milioni 259 zimechangwa katika harambee ya kuendeleza ujenzi wa jengo jipya la Kanisa Katoliki la Mt. Mathayo Mwinjili, Parokia ya Nyamwaga, wilayani Tarime, Mara.

Harambee hiyo ilifanyika katika viwanja vya kiinjili Keisangora - Nyamwaga jana Jumapili, ikiongozwa na mdau wa maendeleo Anitha Gimero Waitara.

Anita ambaye alikuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo, alichangia shilingi milioni 34 na kufanikisha upatikanaji wa kiasi kingine cha shilingi milioni 225 kutoka kwa wageni na waumini wa kanisa hilo.
Anita akichangisha fedha katika harambee hiyo

Miongoni mwa wadau wengine wa maendeleo waliopiga jeki harambee hiyo ni mfanyabishara maarufu wa mjini Tarime, Mama Leah (Agnes Mwita Chacha), Mkurugenzi wa Goldland Hotel, Simon Mseti Wangwe na Mkurugenzi wa Kampuni ya Rubida, Chacha Ernest Mwera, ambao kila mmoja alichangia shilingi milioni 10.

Nayo familia ya wachimbaji wa madini kutoka Buhemba wilayani Butiama ikiongozwa na Timothy Mohabe Gisunte ilitoa mchango wa shilingi milioni 42.
Mmoja wa familia ya wachimbaji madini kutoka Buhemba akizungumza katika harambee hiyo

Wachangiaji wengine na kiasi walichotoa kikiwa kwenye mabano ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara (milioni 1/-), Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete (milioni 1/-) na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles (milioni 2/-).

Akizungumza katika harambee hiyo, Anita ambaye pia ni mzaliwa wa kijiji cha Nyankoni wilayani Tarime na Mkurugenzi wa Kampuni ya Gimero & Sons Ltd, alionesha matumani makubwa kwamba ujenzi wa jengo la kanisa hilo utakamilika.

“Mimi binti yenu (msubati) ninapenda kuwambia kanisa hili litaezekwa na kukamilika kabla ya miaka sita iliyopagwa,” alisema Anita mbele ya mamia ya wageni na waumini wa Parokia ya Nyamwaga.

Aliwashukuru Mama Leah, Wangwe na wadau wote walioshiriki kwa moyo wa upendo na kujitolea kutoa michango kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo hilo la kisasa la ghorofa.
Anita (kushoto) na Mama Leah wakipongezana wakati wa harambee hiyo

“Namshukuru sana Mama Leah na Simon Mseti Wangwe. Pia, nimefarijika sana kwa michango ya familia ya wajimbaji madini na wengine wote, mbarikiwe sana,” alisema Anita.

Aidha, aliwashukuru Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila na Paroko wa Parokia ya Nyamwaga, Padre Julius Manyonyi, kwa kumpa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo.
Mhashamu Askofu Msonganzila akimkabidhi Simon Mseti Wangwe zawadi ya kitambaa cha suti wakati wa harambee hiyo.

Desemba 2023, Anita alishiriki harambee ya kanisa hilo na kutoa fedha kwa jili ya ununuzi wa mabati yote ya kuezeka jengo hilo, lakini zikaelekezwa kwenye shughuli nyingine za ujenzi huo.

“Niliahidi kuezeka kanisa na kutoa mabati yote, lakini pesa ikaelekezwa kwa kazi nyingine, ndio maana Baba Askofu ameridhia mimi nirudi kuchangia. Nasikia faraja sana kuja katika harambee hii ya kuezeka kanisa hii.

“Fr. Paroko, umeniheshimisha nyumbani kwa kuniombea kwa Askofu kuja hapa, hakika nimeuona mkono wa bwana,” alisema Anita.

Simion Kilesi akikabidhi mchango wake wa shilingi milioni mbili.

Kwa upande wake Mhashamu Askofu Msonganzila naye aliwashukuru wadau mbalimbali kwa kuendelea kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ujenzi wa kanisa la parokia hiyo.

Awali, kiongozi huyo wa kiroho aliwakumbusha waamini na wageni wote waliohudhuria harambee hiyo kuendelea kuwa watu wema na kufanya kazi ya Mungu.

Chacha Ernest Mwera (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza mara baada ya kukabidhi mchango wake wa shilingi milioni 10.

Ujenzi wa jengo hilo litakalokuwa na uwezo wa kutumiwa na watu 1,500 kwa wakati mmoja, unatarajia kugharimu shilingi zaidi ya bilioni mbili.

Nao waamini wa kanisa hilo walimshukuru Anitha na wadau wengine kwa kuendelea kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.

“Tunamshukuru Mungu harambee imeenda vizuri, tumepata michango mizuri, tutapiga hatua kwenye ujenzi wa kanisa letu,” alisema mmoja wa waumini wa kanisa hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages