
Picha ya pamoja katika hafla ya uzinduzi wa SOAT JIJINI Arusha juzi
Arusha
---------------
Jumuiya ya Wawekezaji Mahiri katika Maeneo ya Wanyamapori (SOAT) imezinduliwa rasmi jijini Arusha, huku wawekezaji hao wakiahidi kushirikiana na serikali kuendeleza utalii na kuhakikisha ndani ya miaka 20 wanaingizia taifa shilingi bilioni 790 kutokana uwekezaji wao.
Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Arusha juzi, Mtendaji Mkuu wa SOAT, Erasmus Tarimo, alisema wanachama wa jumuiya hiyo wanatarajia kuwekeza katika miradi mbalimbali kwa jamii kwa dola za Kimarekani milioni 50 kwa kipindi cha miaka 20 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 125.
Tarimo alisema kutakuwa na uwekezaji katika ulinzi wa usiopungua dola milioni 20 ili kukabiliana na majangili kwa kipindi cha miaka 20 na uwekezaji katika utafiti dola milioni saba.
Alisema SOAT inatarajia kuimarisha mfumo wa udhibiti ili kuhakikisha usimamizi imara na mazingira yanayotabirika ya uwekezaji wa muda mrefu unaotegemea utalii wa wanyamapori.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, dira yetu sisi ni kuunganisha wanyamapori, jamii na utalii kwa ajili mafanikio endelevu ya kiuchumi na misheni ni kushirikiana kulinda wanyamapori, kuinua jamii katika kuhifadhi na kuendeleza utalii endelevu,” alisema Tarimo.
Alisema malengo ya SOAT ni kuongeza wigo wa chaguo kwa wateja kuhusiana na shughuli za matumizi na sisizo za matumizi, kutekeleza uwekezaji bunifu katika utalii, kuhimiza uwekezaji mbadala, kuendeleza na kutangaza bidhaa za utalii pamoja na kudumisha ubora wa maeneo ya uhifadhi.
“Pia, tunakusudia kuendeleza uwekezaji toshelezi ili kuwekeza katika kujenga miundombinu stahiki katika maeneo ya hifadhi, kuimarisha uhifadhi, manufaa ya kijamii na kiuchumi pamoja na kuzalisha mapato zaidi na kutumia rasilimali za wanyamapori kwa kutoa shughuli mbalimbali endelevu za matumizi ya wanyamapori,” alisema.

Akizindua umoja huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko, alipongeza wawekezaji hao wa Maeneo ya Uwekezaji Mahiri wa Wanyamapori (SWICA) kuanzisha umoja huo ambao utasaidia kuimarisha mawasiliano na serikali.
Semfuko alisema tangu kuanza utaratibu wa SWICA serikali imekuwa ikinufaika na uwekezaji mahiri katika maeneo ya wanyamapori zaidi ya mara tisa kwa sasa.
Alisema mfumo wa uwekezaji mkakati wa SWICA ulianza kutekelezwa kwa kuanzia na wawekezaji sita kwa uwekezaji wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 278 sawa na shilingii za Kitanzania bilioni 696.
Meja Generali Mstaafu Semfuko alisema awali SWICA ilikuwa na wawekezaji sita na sasa wako 13, lakini pia wapo wengine ambao wanataka kuwekeza hatua ambayo inaonesha umuhimu wa uwekezaji huo mahiri katika sekta ya utalii.
Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akifuatilia uwekezaji katika SWICA na anaamini kuwa unakwenda kulinufaisha Taifa, lakini pia kuchangia kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binadamu na kuongeza ajira na mapato.

Awali, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Mlage Yussuf Kabange, alisema maeneo ya SWICA yapo ndani ya maeneo ya TAWA, hivyo SOAT itapewa ushirikiano mkubwa kuhakikisha inafikia malengo yake.
Kamishna Kabange alisema TAWA inaamini ushirikiano ukiimarishwa, lengo la serikali kufikisha watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030 litafanikiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa SOAT, Makamu Mwenyekiti, Martha Lukumaye Baare, alisema wamejipanga kufanya kazi na serikali lakini wanaomba pia kutatuliwa changamoto kadha zikiwemo za kikodi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Mwiba Holdings Ltd ambayo ni miongoni mwa wanachama waanzishilishi wa SOAT, Nicolaus Negri, aliishukuru serikali kufika katika uzinduzi huo na kuahidi SOAT itafanya kazi kwa kushirikiana na serikali.
Negri pia aliewashukuru viongozi wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Chama cha Wawindaji wa Utalii nchini (TAHOA), Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na wadau wengine wa utalii kushiriki katika uzinduzi huo ambao ni muhimu katika kuboresha sekta ya uhifadhi na utalii nchini.
Maeneo ambayo yanawekezwa kupitia SWICA ni eneo la kaskazini la Pori la Akiba Maswa, Maswa Kimali, Maswa Mbono, Mapori ya Akiba Grumeti na Ikorongo, Pori la Akiba Mkungunero, Pori Tengefu la Ziwa Natroni na Kitalu cha LL1 katika Pori la Akiba Selous.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment