
Nyambari Nyangwine (aliyevaa kofia) akiwa na ujumbe wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam juzi, tayari kwa safari ya kuelekea China kwa ziara ya kibiashara ya siku 11.
Dar es Salaam
---------------------
Mfanyabiashara wa Tanzania, Nyambari Nyangwine ameanza ziara ya kibiashara ya siku 11 nchini China.
“Nitakuwa na ziara ya kibiashara nchini China kwa siku 11, na miongoni mwa miji ambayo nitatembelea ni Shangai na Guangzhou,” amesema Nyambari.
Nyambari ambaye pia ni mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini alikuwa akizungumza na Gazeti la Sauti Mara jijini Dar es Salaam, juzi muda mfupi kabla ya kupanda ndege pamoja na ujumbe wake kuelekea China.
Nyambari ambaye ni Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies Ltd (NNGCL), amekuwa akitanua uwekezaji wake ndani na nje ya Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.
Mfanyabiashara huyo pia ni mwanasiasa ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime kupitia chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakati huo huo, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA limeitunuku Nyambari Nyangiwne Group of Companies Ltd cheti maalum cha shukurani, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake wa udhamini uliosaidia kufanikisha Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani.

Mwakilishi wa Nyambari Nyangwine Group akionesha cheti cha shukurani walichotunukiwa na BAKITA
Nyambari Nyangwine Group ilikabidhiwa tuzo hiyo wakati wa kongamano hilo ambalo lilifanyika Machi 24 hadi 27, 2026 katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Wadhamini wa Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani, akiwemo mwakilishi wa Nyambari Nyangwine Group katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment