
Noela Gachuma (kushoto) akizungumza katika hafla ya Usiku wa Mwana mke Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, jana Machi 28, 2026.
Rorya
--------------
Wanawake wamehimizwa kujitambua, ikiwemo kujiunga kwenye vikundi na kuchangamkia fursa za kiuchumi ili kujiletea maendeleo kwa manufaa ya jamii kwa ujumla.
Hamasa hiyo ilitolewa jana Machi 28, 2026 na mgeni rasmi katika hafla ya Usiku wa Mwanawake Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Noela Gachuma, iliyokuwa sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani 2026.
Katika hotuba yake, Noela alisisitiza nafasi ya mwanamke katika malezi ya watoto, akisema watoto ni hazina na viongozi wa kesho, hivyo ni jukumu la mama kuhakikisha wanalelewa katika misingi ya kimaadili.
Aliongeza kuwa familia imara huanza na ndoa inayoheshimiwa, kuthaminiwa na kulindwa kikamilifu.
“Watoto ni hazina na viongozi wa kesho, jukumu la kulea watoto ni la kwetu akina mama. Ndoa iheshimiwe na itunzwe. Ukiwa na mume wako mlinde kama unavyolinda mboni ya jicho lako,” Noela alisisitiza.
Kuhusu jitihada za kujikwamua kiuchumi, Noela aliwakumbusha wanawake kutokata tamaa wanapokutana na changamoto za maisha, akisema mafanikio yanahitaji ujasiri na uthubutu.
“Fedha inatafutwa lakini fedha inaheshimiwa, usiogope na usione aibu, unapopata changamoto usijifiche - pambana ili utoke kwenye changamoto usonge mbele,” alisema.
Noela alitumia nafasi hiyo pia kutoa rai kwa wanawake kutumia mikusanyiko kama hiyo kuungana, kubadilishana mawazo na kusaidiana.
“Tunapokutana hapa tutengeneze network (mtandao), siri kubwa ya mafanikio ni kutengeneza network, networking ni kitu cha muhimu sana kwenye maisha ya utafutaj,” alisema Noela.
Katika hatua nyingine, Noela alikemea vikwazo vinavyowakwamisha wanawake kiuchumi, akibainisha kuwa mojawapo ni wanaume wanaowazuia wanawake kufanya kazi za kujipatia kipato.
“Adui wa mwanamke ni mwanaume anayemzuia mwanamke kutoka kwenda kufanya kazi,” alisema.
Akihitimisha hotuba yake, Noela aliwahimiza wanawake kujiunga na vikundi vya kiuchumi ili kunufaika na mikopo inayotolewa na halmashauri kutokana na fedha zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nawakumbusha wanawake kujiunga kwenye vikundi ili kupata fedha za Mama Smaia ambazo zinapatikana halmashauri na mziwekeze sehemu ambazo ni salama,” alisema Noela.
Hafla hiyo ya Usiku wa Mwanamke Wilaya ya Rorya ilihitimishwa kwa Noela Gachuma kutunukiwa cheti cha pongezi kwa mchango wake katika kuhamasisha maendeleo ya wanawake, huku washiriki wakiondoka wakiwa na ari mpya ya kuchangamkia fursa za kujikwamua kiuchumi.

Noela Gachuma (katikati) akikabidhiwa cheti cha pongezi. (Picha zote na Mpigapicha Wetu)

No comments:
Post a Comment