NEWS

Tuesday, 31 March 2026

Waziri Mkuu Mwigulu: Lukuvi atakumbukwa kwa kujali maisha ya wananchi



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akiweka shada la maua kwenye kaburi la William Lukuvi kijijini Idodi, wilayani Iringa, leo Machi 31, 2026.

Na Mwandishi Wetu
Iringa
---------------

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Machi 31, 2026 ameongoza mamia ya wananchi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa JImbo la Isimani, William Lukuvi.

Mazishi hayo yamefanyika nyumbani kwa Lukuvi katika kijiji cha Idodi kilichopo wilaya ya Iringa, mkoani Iringa.

Akizungumza katika mazishi hayo, Waziri Mkuu Mwigulu amesema atakumbukwa na Watanzania kwa mambo mengi kutokana na utumishi wake uliotukuka katika nafasi mbalimbali alizohudumu serikalini.

“Mheshimiwa Lukuvi atakumbukwa kwa mengi na Watanzania kutokana na utumishi wake uliotukuka katika nafasi mbalimbali. Mchango wake kwa jamii na Watanzania kwa ujumla katika nafasi mbalimbali alizotumikia kuanzia chama, jimboni na serikalini umekuwa chachu katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nitumie nafasi hii kuwahahikishia kwamba jinsi alivyokuwa pamoja nanyi wakati wa uhai wake na yale yaliyokuwa ndoto yake, yataendelea kutimizwa.

“Ni vema tukizingatia na kuyaishia yale tuliyoelezwa na viongozi wa dini pamoja na kwenye wasifu wake. Alikuwa akisisitiza ushirikiano baina ya Bunge na Mawaziri, leo hii tuyaenzi yote aliyoyasimamia.

“Na kwa wana-Isimani, ninawasihi tuendelee kumuenzi, tusianze mashindano, tulinde heshima ya mzee wetu kwa kuwa na staha,” amesema Waziri Mkuu Mwigulu.

Ameongeza kuwa Lukuvi alikuwa anajali maisha ya anaowaongoza, ndiyo maana ameweza kudumu jimboni kwa miaka 31.

“Sisi wanasiasa tunajua, siyo kazi rahisi kuongoza kwa muda wote huo, lakini yeye aliweza kwa sababu aliweka kipaumbele chake kwenye maisha ya wale anaowaongoza,” amesema.


Waziri Mkuu Mwigulu akiipa pole na kuifariji familia ya Lukuvi

Waziri Mkuu huyo amesema serikali itaendelea kumuenzi Lukuvi kwa kuendelea kutekeleza miradi aliyoiacha, hasa wa barabara ya lami ambayo alikuwa anaifuatilia kwa karibu.

“Miradi ya Pawaga na Isimani yote itakamilishwa. Niwahakikishie kuwa serikali itaendelea kuitekeleza kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, lakini pia sehemu ya kumuenzi Mheshimiwa Lukuvi,” amesema Waziri Mkuu Mwigulu.

Naye Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu, amesema kifo cha Lukuvi kimeacha majonzi kwa kila mmoja na kwa uzito wa msiba huo, Bunge limewakilishwa na wabunge 160.

“Mheshimiwa Lukuvi alikuwa anaujua uwezo wake na kifo chake ni pigo ambalo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepata kwa kuukosa umahiri wake Bungeni,” amesema Spika Zungu.

Mapema, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, ametoa wito kwa vijana wa CCM kujifunza na kuiga mapito ya Lukuvi ambaye alianzia ngazi za chini kabisa hadi akafika kwenye uongozi wa taifa.

“Mwaka 1974 alijiunga na chama cha TANU, akajiendeleza hadi kufikia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana,” amesema Wasira.

Amesema jambo kubwa la kujifunza kutoka kwa Lukuvi ni jinsi alivyoweza kulea jimbo la Isimani ilhali ana majukumu makubwa ya kitaifa.

“Siyo wengi ambao anakuwa Mbunge au Waziri halafu analea jimbo. Watu aina hii wako wachache sana. Wengi wakipata vyeo wanasahau majimbo na kuja kuwaona wapigakura wakati wa uchaguzi,” amesema na kushangiliwa.

Wasira amesema kitendo cha Lukuvi kuweza kudumu kwenye madaraka na marais wanne kuanzia kwa Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Dkt. John Pombe Magufuli hadi sasa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni ishara tosha kwamba aliaminiwa na kuna jambo la kujifunza kutoka kwake.

“Marais wote hawa walikuwa na watu wao, lakini kwa kuendelea kuwa naye, ina maana alikuwa na sifa na uwezo,” amesema Wasira.

Ibada ya mazishi hayo ya Lukuvi imeongozwa na Naibu Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Padre Paul Msombe, ambaye amesisitiza kuwa ni vema watu wakaishi huku wakijiandaa kwa maisha ya baadaye mbinguni.

Padre Msombe amesema: “Licha ya vyeo vyake, alikuwa na unyenyekevu na mwenye kushirikiana na waumini wenzake. Tukumbuke kwamba ipo siku tutalala usingizi kama ndugu yetu William alivyolala usingizi wa amani.

“Kitu cha msingi ni kujiweka mikononi mwa Mungu, tufe katika Bwana. Hili ni suala la kila mmoja kujitazama na kujihoji kwamba mimi Mungu akiniita sasa hivi, ninaweza kusema nina haki ya kuingia mbinguni.?”

Lukuvi alifariki dunia Machi 25, 2026 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mk4eapa mkoani Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages