NEWS

Sunday, 29 March 2026

Wasira: Tufanye maendeleo ya nchi kwanza, uchaguzi wa urais mwaka 2030 uko mbali



Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira.

Na Mwandishi Wetu
Bunda
--------------

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ameonya vikali wanachama wa chama hicho wanaoanza mapema kupanga safu za kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030.

Wasira alitoa karipio hilo Machi 29, 2026 wakati alipokwenda kuweka jiwe la msingi ujenzi wa ofisi mpya ya CCM Wilaya ya Bunda, mkoani Mara.

Alisema ni ajabu kuona na kusikia baadhi ya wanachama wakianza kuzungumzia mbio za urais wa mwaka 2030 wakati taifa limetoka kwenye uchaguzi mkuu miezi michache iliyopita.

“Nimeambiwa wengine wanazungumza urasi wa mwaka 30 [mwaka 2030] leo, tumemaliza uchaguzi mwaka jana [Oktoba 2025], si tujenge kwanza nchi - tufanye maendeleo,” alisema kwa msisitizo.

Aliendelea kuwanyooshea kidole wanaowaza urais wa mwaka 2030 badala ya kujikita katika maendeleo ya taifa na ujenzi wa chama hicho tawala.

Wasira aliwakumbusha watu hao kutambua kwamba hakuna mwenye uhakika wa maisha ya kesho. “Unazungumzia urais wa mwaka 30, wewe umesema na Mungu kwamba utakuwepo?” alihoji.

Aliwataka wana-CCM wote kuelekeza nguvu zao katika kuimarisha chama kuelekea chaguzi za ndani zijazo, akisisitiza kuwa uimara wa chama ndio utakaoamua mafanikio ya uchaguzi mkuu ujao.

“Unaacha kuzungumza mambo yaliyopo ya kutekeleza ilani ya kujenga upya chama unaanza kuzungumza urais: naunga mkono fulani, unamuunga mkono nani amekwambia atakuwepo, au wewe utakuwepo?

“Acha hiyo, twende tujenge chama kuelekea uchaguzi [uchaguzi ujao wa viongozi wa CCM], halafu uchaguzi huo utusaidie kutupa chama chenye nguvu kuelekea mwaka 30 [2030].

“Nani atakuwa rais, Mungu ameshamjua, maana Mungu alitujua kabla dunia haijaumbwa, hawezi kushindwa kujua rais,” Wasira alisisitiza.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages