NEWS

Sunday, 29 March 2026

Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania latunukiwa Tuzo ya Malkia wa Nguvu 2026



Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly, akifurahia Tuzo ya Malkia wa Nguvu 2026 iliyotolewa na Clouds Media Group, hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
------------------------

Shirika lisilo la kiserikali linaloendeleza mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, ukiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni, Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) lenye makao makuu mkoani Mara, limetwaa Tuzo ya Malkia wa Nguvu 2026.

Tuzo hiyo ilitolewa na Clouds Media Group hivi karibuni jijini Dar es Salaam kutambua mchango na juhudi zinazofnaywa na shirika hilo katika kupiga vita vitendo vya ukeketaji mkoani Mara.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly, alisema “Napenda kuishukuru Clouds Media Group kwa kuendesha programu hii na kutunuku shirika langu mwaka huu.

Rhobi alisema na yeye kwa heshima kubwa anapenda kuitunuku tuzo hiyo kwa wadau (partners) wa shirika hilo waliopo ndani na nje ya Tanzania.

“Mimi binafsi naitunuku tuzo hii kwa wadau wetu wa ndani na nje kwa kutufadhili kwa hali na mali ili kutimiza malengo ya shirika,’’ alisema Rhobi ambaye pia ni mwanzilishi wa shirika hilo.

Aliwataja wadau hao kuwa ni Tanzania Development Trust-UK Charity, Netzwerk Rafael- Germany, Polish Aid, Kiabakari Foundation na Hope for Girls and Women- France, French Embassy- Tanzania na FAWCO Foundation.

Alitaja wadau wengine kuwa ni Grumeti Reserves, Mapito Camp, Four Seasons Hotels, Nomad Tanzania, June Powell, UNFPA/C-Sema, ACP- France, Wojiciech Adam, Koscielniak, Julian na Ann Marcus.

Rhobi aliwashukuru pia wafanyakazi wa HGWT na wote waliohudumiwa na shirika hilo, viongozi wa serikali, hasa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dawati la Jinsia Polisi, Mkuu wa Mkoa wa Mara na Wakuu wa Wilaya kwa ushirikiano mkubwa walioonesha kusaidia shirika kutekeleza majumu yake.


Rhobi Samwelly (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa HGWT, Domina Mabebe, wakifurahi baada ya shirika hilo kutunukiwa Tuzo ya Malkia ya Nguvu 2026.

Takwimu zinaonesha mkoa wa Mara umepiga hatua ya kupunguza vitendo vya ukeketaji kutoka asilimia 32 kwa miaka 2010-2017 hadi asimilia 28 kwa miaka 2022-2026 kutokana na juhudi zinazofanywa na shirika la HGWT kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine.

Taarifa zilizopo zinaonesha shirika la HGWT limeokoa wasichana 4,481 waliokuwa katika hatari ya kukeketwa kwa nguvu katika mkoa wa Mara kati ya mwaka 2017 na 2025.

Wasichana hao walipata hifadhi katika nyumba salama ambazo zinamilikuwa na kuendeshwa na shiirka la HGWT katika wilaya za Serengeti na Butiama, mkoani Mara.

Wakiwa katika nyumba salama hizo, wasichana hao pia walipata huduma mbalimbali kama vile msaada wa kisaikolojia, huduma za kiafya, kuendelezwa kielimu na msaada wa kisheria.

Baadhi ya wasichana hao tayari wamehitimu vyuo vikuu, vyuo vya kati, ufundi, elimu za sekondari na msingi.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages