NEWS

Sunday, 22 March 2026

TAKUKURU Mara ilivyofuturisha wadau wa mapambano dhidi ya rushwa



Picha ya pamoja ya viongozi wa dini na serikali, na baadhi ya waamini wakati wa futari iliyoandaliwa na TAKUKURU Mkoa wa Mara, Machi 18, 2026.

Na Godfrey Marwa
Musoma
-------------------

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara, Machi 18, 2026 ilifuturisha wadau wa mapambano dhidi ya rushwa ambao ni Waislamu na Wakristo, ikilenga kuonesha upendo na kuimarisha ushirikiano uliopo baina yao.

Futari hiyo ilifanyika mjini Musoma na kuhudhuriwa makundi mbalimbali, wakiwemo waamini wa madhehebu hayo, kamati ya maridhiano ya mkoa huo, wazee maarufu, watu wenye mahitaji maalum, maafisa usafirishaji na viongozi wa serikali.

Akizungumza wakati wa futari hiyo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Dkt. Khalifan Haule, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara kama mgeni rasmi, alihimiza umuhimu wa kudumisha amani katika jamii.

"RC amenieleza kuwa nizungumzie umuhimu wa amani… amani ndiyo msingi wa kila kitu, tuhakikishe tunahubiri amani kwenye nyumba zetu za ibada, bila amani hatuwezi kupata nafasi ya kufanya shughuliza, ibada,” alisema na kuongeza:

"Tuhamasishe upendo na mshikamano kwa waamini wetu, tuendelee kuombea viongozi wa kitaifa na serikali, na hasa Rais Samia, Mwenyezi Mungu amjaalie afya njema ampe afya njema, ampe umri mrefu aendelee kutumikia kwa haki na amani tuweze kupata maendeleo.”

Naye Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Saimon Ngoma, akiwasilisha salamu za taasisi hiyo aliwashukuru wadau hao kutokana na ushirikiano wao uliopelekea mapambano dhidi ya rushwa kufanikiwa.

"Nitumie fursa hii kuwashukuru viongozi na wadau wote kwa ushirikiano mnaotupatia katika utendaji, jambo ambalo linawezesha mapambano dhidi ya rushwa Mara kuwa ya kufanikiwa.

"Tumekuwa tukishirikiana katika kutoa elimu, kufanya uchunguzi, lakini pia kwa kufuatilia matumizi ya fedha za serikali zinazotumika katika miradi ya maendeleo,” alisema Ngoma.

Aliongezea kuwa wao ni sehemu ya jamii ndiyo maana wakati mwingine wanaonekana wakitoa misaada mbalimbali ya kijamii, ikiwemo kukabidhi mashine mbili za kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti) katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Aidha, wadau hao walieleza kuridhishwa na utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Mara.

"Tunashukuru baadhi ya maeneo kwenye ofisi za serikali kuna unafuu, tumekuwa tukipokelewa vizuri, hakuna tena habari ya mtu kukuzungusha nyuma ya nyumba kwa sababu wako macho sana.

"Niwaombe waendelee kufanya kazi hiyo kwa weledi ili kuokoa masikini ambao ndio wengi,” alisema mmoja wa waamini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages