NEWS

Wednesday, 1 April 2026

Vita ya Marekani, Israel dhidi ya Iran yatatwa kuathiri gharama za uagizaji mafuta, EWURA yatangaza bei mpya




Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazoanza kutumika nchini kuanzia leo Jumatano, Aprili 1, 2026.

EWURA imechukua hatua hiyo kutokana na ongezeko kubwa la bei ikibainishwa kuwa ni kutokana na athari za mzozo wa kivita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran ulioibuka Februari 28, 2026.

Katika taarifa yake, EWURA imeeleza kuwa mashambulizi katika visima vya mafuta, maghala na viwanda vya kusafisha mafuta Mashariki ya Kati, na kufungwa kwa Lango la Hormuz - linalopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta duniani, vimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la duniani, hivyo kuathiri pia gharama za uagizaji nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa bei mpya, Dar es Salaam sasa Petroli ni shilingi 3,820, Dizeli (3,806) na Mafuta ya Taa (3,684).

Tanga bei mpya ya Petroli ni shilingi 3,881, Dizeli (3,867) na Mafuta ya Taa (3,745).

Mtwara bei ya Petroli ni shilingi 3,912, Dizeli (3,898) na Mafuta ya Taa (3,777), huku maeneo mengine nchini Petroli ikiwa shilingi zaidi ya 4000.

EWURA imesisitiza kuwa wafanyabiashara wote wa mafuta nchini wanapaswa kuuza kwa bei zinazooneshwa kwenye mabango ya vituo vya mafuta, na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka.

Aidha, mamlaka hiyo imewataka wananchi kutumia mafuta kwa uangalifu na ufanisi kutokana na athari za kimataifa zinazoendelea, huku ikiendelea kuchukua hatua za kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini hauathiriki.

Bei hizo mpya zimepanda ikiwa ni tofauti na Bei zilizotangazwa Machi 4, 2026 ambapo maeneo mengi nchini ilikuwa shilingi 2864 hadi 2959.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages