NEWS

Wednesday, 25 March 2026

Waziri Mwandamizi William Lukuvi afariki dunia, Rais Samia amlilia



William Lukuvi enzi za uhai

Na Mwandishi Wetu

Mmoja wa mawaziri waandamizi katika Serikali ya Tanzania, William Vangimembe Lukuvi, amefariki dunia leo Jumatano asubuhi jijini Dodoma.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka, imeeleza kuwa Waziri huyo wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) alipatwa na umauti wakati akipatiwa matibabu ya mshituko wa moyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Lukuvi amekuwa mbunge kwa kipindi cha miaka 30 kabla ya kuchaguliwa tena Oktoba 2025 kwa kipindi kingine cha awamu ya saba.

Alibahatika kushika cheo cha uwaziri katika awamu za marais Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, John Magufuli na Samia Suluhu Hassan.

Taarifa ya Ikulu imesena Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametangaza habari za kifo cha Waziri Lukuvi, amehuzunishwa na msiba huo na kutoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki.

Watu wa karibu na waliofanya kazí na Lukuvi wamemweleza kuwa alikuwa mchapakazi, mwadilifu, mpenda watu, asiyependa uonevu na aliyechukia rushwa.

Wanasema sifa hizo ndizo zilizomwezesha kuaminiwa na marais waliomteua kuwa ama Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa na hatimaye kupanda ngazi ya kuwa waziri katika awamu tofauti za marais waliopita.

Katika awamu hii ya Rais Samia, Lukuvi ndiye alikuwa waziri mwandamizi kupita wengine waliomfuata.

Serikali kwa kushirikiana na Ofisi wa Bunge na familia  wanaandaa mazishi ya mwanasiasa huyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages