NEWS

Sunday, 5 April 2026

Askofu Maswi: Umaskini ni laana, wezi wa zaka watakufa maskini



Askofu Joshua Maswi

Na Christopher Gamaina
Tarime
----------------

Askofu wa Kanisa la EAGT Tarime Mjini, Joshua Maswi, amesema umaskini si mpango wa Mungu kwa mwanadamu, bali ni moja ya laana ambazo zilipaswa kuondolewa kupitia kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.

Akihubiri katika ibada ya Jumapili ya Pasaka kanisani hapo leo Aprili 5, 2026, Askofu Maswi ameeleza kuwa kupitia kifo cha Yesu msalabani, mwanadamu amepewa maisha ya ushindi na ustawi, si ya mapungufu.

“Umaskini ni laana, na laana zote hazitakiwi kutenda kazi katika maisha yetu [binadamu]. Yesu alikufa maskini ili tuwe matajiri,” amesema huku akiwatazama waumini waliokuwa wakimsikiliza kwa makini.

Askofu Maswi ameongeza kuwa si umaskini tu uliobebwa na kifo cha Yesu, bali pia laana za magonjwa na mateso ya aina zote.

“Yesu alimaliza laana zetu za magonjwa na umaskini kwa kifo chake msalabani, umaskini hautakiwi kabisa. Yesu anataka tufanikiwe katika mambo yote. Mapungufu yote hutakiwi kuwa nayo,” amesisitiza.

Aidha, amewakumbusha waumini umuhimu wa utii katika mambo ya Mungu, hasa suala la utoaji wa zaka, akionya kuwa wanaokiuka kanuni hiyo wanajiweka katika hatari ya kubaki kwenye hali ya umaskini.

“Wezi wa zaka watakufa maskini,” kiongozi huyo wa kiroho ameonya akisisitiza kuwa baraka za Mungu zinahitaji uaminifu na utii kamili.

Mahubiri hayo ya Askofu Maswi yametanguliwa na maombi, shukrani na nyimbo za sifa katika ibada hiyo ya Jumapili ya Pasaka.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages