NEWS

Tuesday, 14 April 2026

Dkt. Kessy Mkuu mpya wa TANAPA Kanda ya Kaskazini



Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga (aliyevaa shati jeupe) akikabidhi ofisi ya TANAPA Kanda ya Kaskazini kwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Dkt. Beatrice Kessy, jijini Arusha, leo Aprili 14, 2026.

Na Mwandishi Wetu

Arusha
---------------

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limendelea kuwaamini na kuwapa wanawake nafasi za juu katika uongozi - kwa kumteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Dkt. Beatrice Kessy kuwa Mkuu wa shirika hilo Kanda ya Kaskazini.

Dkt. Kessy amechukua nafasi ya mwanamke mwenzake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga ambaye amestaafu.

Hafla ya makabidhiano ya ofisi ya Kanda ya Kaskazini yenye hifadhi tano imefanyika leo Aprili 14, 2026 makao makuu ya Kanda ya Kaskazini yaliyopo Majengo, jijini Arusha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Kamishna (mstaafu) Ndaga amesema watumishi wa kanda hiyo wana ushirikiano, nidhamu, weledi na wasiosukumwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Naondoka nakuachia ofisi iliyojaa watumishi wenye ushirikiano, kiu ya maendeleo na tuliofanya nao kazi bila kusukumana na kujenga msingi wa mafanikio ya pamoja ambayo leo yanatupa sifa ndani ya kanda yetu ya kaskazini," amesema Ndaga.

Kwa upande wake, Dkt. Kessy ameahidi kushirikiana na watumishi kuhakikisha hifadhi za kaskazini zinaimarisha uhifadhi na kuongoza katika makusanyo ya mapato, kutangaza utalii na vivutio vilivyopo, sambamba na uboreshwaji wa miundombinu ya hifadhi.

"Ushirikiano huu mliouonesha awali na udumishwe zaidi ili kuboresha mazingira rafiki ndani ya hifadhi zetu tano za kanda hii kuwa vinara wa ukusanyaji mapato, utalii na miundombinu - ambapo tutapata fursa ya kuwavutia wageni wengi na kujinyakulia tuzo katika anga za kitaifa na kimataifa," amesema Dkt. Kessy.

Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages