NEWS

Tuesday, 7 April 2026

Fedha za CSR Barrick North Mara zawezesha vikundi vya vijana kiuchumi



Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmshauri ya Wilaya ya Tarime, Anthony George Nyange.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
--------------

Shilingi milioni 220 kutoka mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara zimeelekezwa kuwezesha vikundi 13 vya vijana kuanzisha miradi ya kiuchumi katika vijiji vyote 11 vinavyozunguka mgodi huo.

Tayari vikundi hivyo vimepokea fedha hizo, ikiwa ni ruzuku ya CSR ya mwaka uliopita kutoka mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Kwa mujibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, fedha hizo zimesaidia vijana takriban 100 wanachama wa vikundi hiyo kuanzisha miradi ya kiuchumi.

“Nawashukuru sana Barrick, hususan idara ya mahusiano kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitoa katika kufanikisha mpango huu wa ruzuku ya CSR kwa vajana,” Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jami wa halmashauri hiyo, Anthony George Nyange, aliwambia waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni.

Nyange alisema miradi hiyo imesaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa katika viijiji hivyo kwa ajili ya ustawi wa jamii inayouzunguka mgodi huo.

“Wanufaika wengi ni vijana na wamejielekeza kwenye miradi ambayo siyo tu kwa ajili ya kijipatia kipato bali pia kutatua changamoto zilizokuwepo,” alisema Nyange.

Alitaja vikundi ambavyo vimenufaika na mpango huo kuwa ni Mokarambe Agribuness, Hope and Revolution of Economy for Youth, Tunza Mazingira Nyamongo, Amshana Nyamongo na REMHOCHI.

Viingine ni Kazi ni Moyo, Konna Nne, Kiumanya, Ibuka Umoja, Tunaweza Kerende, Nyasa Group, Mtanzamo Youth na Kikundi cha Keryoba.

Alisema baadhi ya vikundi hivyo vimeanzisha miradi ya usafi wa mazingira jambo ambalo limesaidia kuuweka mji mdogo wa Nyamongo katika hali nzuri ya usafi.

“Kwa mfano, kulikuwa na changomoto ya usafi katika mji wa Nyamongo, sasa hali ya usafi ni nzuri kwa sababu kuna kikundi cha mazingira ambacho kinafanya vizuri sana kwenye usafi wa mazingira,” alisema Nyange.

Nyange alisema Halmashauri ya Wilaya ya Tarime itaendelea kutenga sehemu ya fedha za CSR kwa ajili ya kuwezesha vijana kuanzisha na kuendeleza miradi ya kiuchumi.

“Tunategemea na mwaka huu pia tutatenga sehemu ya CSR kwenda kuwezesha vijana kwenye miradi ya kiuchumi.

“Sasa hivi, vijana wengi kule Nyamongo wana shughuli za kufanya kujipatia kipato na hata vitendo vya kihalifu vimepungua,” alisema Nyange.

Alisema mbali na mpango wa CSR, vijana hao pia wamenufaika na mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na halmshauri hiyo kuwezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Wanufaika wakubwa ni vijana, na mbali ya kunufaika na mikopo yetu ya halmashauri ya asilimia 10, pia wamenufaika na mpango wa ya ruzuku ya CSR kwa vijana,” alifafanua Nyange.

Taarifa zinaonesha Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inaongoza kwa kutoa kiasi kikubwa cha mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika mkoa wa Mara.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages