NEWS

Tuesday, 7 April 2026

Tume ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29 yaongezewa muda



Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman

Na Mwandishi Wetu
---------------------------

Mamlaka ya Uteuzi imeridhia maombi ya muda wa ziada kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hivyo imeiongezea tena muda wa siku 21 na kuitaka ikamilishe kazi hiyo kabla au ifikapo Aprili 24, 2026.

Mamlaka hiyo imeeleza sababu za kuongeza muda huo kwa Tume hiyo kuwa ni pamoja na kuiwezesha kukamilisha uchambuzi wa ushahidi, taarifa na maoni yaliyopokewa na kutoa fursa kwa wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi kufanyia kazi baadhi ya vielelezo vipya vilivyowasilishwa.

Sababu nyingine ni kuiwezesha Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, kukamilisha maandalizi ya ripoti itakayowasilishwa kwa Rais.

Tume hiyo ilianza kutekeleza majukumu yake Novemba 20, 2025 na ilitarajiwa kukamilisha kazi yake ndani ya kipindi cha siku 90.

Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali, Tume hiyo iliongezewa muda wa kukamilisha kazi na kutakiwa kuwasilisha ripoti kwa Rais kabla au ifikapo April 3, 2026.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages