NEWS

Wednesday, 29 April 2026

Tanzania yang’ara kimataifa kwa mchango wa madini unaokuza pato la taifa




Nairobi, Kenya
----------------------

Sekta ya madini nchini Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa baada ya kupongezwa kwa mchango wake mkubwa katika kukuza pato la taifa (GDP), huku nchi jirani zikieleza nia ya kujifunza mafanikio ya usimamizi wa sekta hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa Madini (Kenya Mining Investment Conference and Expo - MICE) 2026, unaofanyika jijini Nairobi, Kenya, Aprili 28 hadi 29 Aprili 2026 na kuhudhuriwa na viongozi, wawekezaji na wadau wa sekta ya madini barani Afrika.

Wakizungumza katika mkutano huo, mawaziri mbalimbali wadini wa Afrika wameeleza kutambua hatua kubwa zilizopigwa na Tanzania katika kuifanya sekta hiyo kuwa mhimili wa uchumi.

Waziri wa Madini wa Tanzania, Anthony Mavunde, amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kusukuma mbele ajenda ya kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi.
Waziri Mavunde akizungumza katika mkutano huo

Awali, akifungua mkutano huo, Rais wa Kenya, William Ruto, amezitaka nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla kuunganisha nguvu katika kuongeza thamani ya rasilimali madini ili kuongeza tija na ushindani wa ukanda huo katika soko la dunia.

Akihitimisha, Waziri Mavunde amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuichangamkia Tanzania, akieleza kuwa ipo tayari kupokea uwekezaji katika maeneo ya uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini, sambamba na kuwepo kwa sera na miundombinu rafiki kwa biashara.

Katika kuonesha imani kwa Tanzania, nchi za Kenya, Somalia na Sudan Kusini zimesema zinaendelea kujifunza kutoka kwa Tanzania, hususan katika mifumo ya usimamizi, uongezaji thamani na ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo katika uchumi wa madini.

Katika mjadala huo, Waziri wa Madini, Uchumi wa Bluu na Masuala ya Bahari wa Kenya, Hassan Ali Joho, ameitaja Tanzania kama mfano bora wa kuigwa kikanda, akisisitiza kuwa ushindani siyo kipaumbele bali ushirikiano wa pamoja ili kukuza na kuimarisha sekta ya madini barani Afrika.

Naye Waziri Waziri wa Petroli na Rasilimali Madini wa Serikali ya Shirikisho ya Somalia, Dahir Shire Mohamed, amesema nchi yake inaichukulia Tanzania kama mfano halisi katika kujenga mifumo imara ya usimamizi wa rasilimali madini na kuwa Somalia inaendelea kujifunza kutoka Tanzania.

Viongozi wengine ambao wameshiriki katika mjadala huo ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Madini Imara wa Nigeria, Oladele Henry Alake na Waziri wa Madini wa Sudan Kusini, Losuba Ludoru Wongo.

Kwa pamoja, mawaziri hao wamejadiliana kuendeleza ushirikiano wa kikanda, huku wakisisitiza kuwa bara la Afrika linaweza kujenga uwezo wa pamoja na kunufaika zaidi na rasilimali zake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages